Habari za Kitaifa

Nimeachia Mungu, Gachagua asema akizidi kusakamwa

Na JUSTUS OCHIENG' Na BENSON MATHEKA September 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANDANI wa Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua waliendeleza malumbano kati yao Jumapili, Septemba 22, 2024 huku mbunge mmoja akidai kuwa hoja ya kumtimua naibu rais imeiva.

Hata hivyo, Bw Gachagua alisema licha ya vitisho vya kuondolewa mamlakani ana imani kuwa ameachia Mungu ashughulike jinsi alivyoshughulikia Rais William Ruto alipohujumiwa chini ya utawala wa Jubilee.

Akisisitiza kuwa hakuna mswada unaoweza kuwasilishwa bungeni bila idhini ya rais na kwamba kiongozi wa nchi aliahidi kuwa hatakubali naibu wake ateswe alivyofanyiwa, Bw Gachagua alisema Mungu aliyemnusuru Ruto wakati alipoteswa angali enzini.

“Yule Mungu aliyekuwepo alipoahidi kuwa hatakubali naibu wake ateswe na yule aliyekuwepo alipokuwa akihangaishwa akiwa naibu rais, huyo Mungu bado yuko,” alisema Bw Gachagua akiwa katika ibada ya kanisa Thika.

Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba alidai kuna mpango wa kuwasilishwa bungeni kwa hoja hiyo wiki ijayo.

“Inasikitisha kuwa rais ameungana na marafiki wake wapya wa ODM na wiki ijayo wanapanga kuwasilisha hoja ya kumwondoa afisini Naibu Rais. Tunataka kumwambia Rais aheshimu kura alizopata kutoka Mlima Kenya na akomeshe njama chafu dhidi ya naibu rais,” akasema Bi Wamuchomba.

Aliongea katika Kanisa la PEFA mjini Thika, kaunti ya Kiambu alikoshirikiana na wandani wengine wa Bw Gachagua kumtetea.

Akiongea mahala tofauti, Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alijibu kwamba naibu rais “alijiondoa afisini mwaka mmoja uliopita” akiongeza kuwa kile wabunge watafanya ni kurasimisha hatua hiyo kupitia kura bungeni “kabla ya mwaka huu kuisha.”

“Hakuna mbunge amehongwa. Tumeamua kuweka kando ukabila na kuapa kwamba kabla ya mwisho wa mwaka huu, Rigathi Gachagua, Naibu Rais wa Kenya atasherehekea Krismasi kama raia wa kawaida ili aendeleze mikutano yake ya kikanda kule vijijini,” akasema Bw Barasa.

Lakini wandani wa Bw Gachagua wameshikilia kuwa wako tayari kuzima hoja hiyo ya kumtimua afisini.

Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya alisema inasikitisha kuwa wakazi wa Mlima Kenya walikaidi ushauri wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwamba wasimuunge mkono Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mlima Kenya ulikaidi Uhuru na kukubali kumlipa Ruto deni la kisiasa. Sharti tujifunze kwamba kila mara ni vizuri kulipa wema na matendo mema. Nataka kumwambia Rais kwamba asihasau marafiki zake wa zamani eti kwa sababu amepata marafiki wapya. Marafiki zako leo walikuwa maadui wako. Usiwasahau marafiki zako wa zamani waliokusaidia,” Mbunge huyo alisema.

Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru almaarufu Mejja Donk, alisema inasikitisha kuwa shida kubwa ya viongozi nchini Kenya ni kufeli kutimiza ahadi zao.

“Uhuru alituonya dhidi ya kumpigia kura Ruto. Alibashiri kuwa tutalia baada ya miaka miwili. Inasikitisha kuwa wakati huu hatuzungumzi kuhusu maendeleo bali maovu ambayo wewe Rais Ruto unamtendea naibu wako na watu wa Mlima Kenya,” Bw Gathiru akasema.

Akaongeza: “Una mamlaka na kila kitu lakini sisi tuna Mungu aliye Mbinguni. Hauwezi kuendelea kudanganya Wakenya. Leta hoja ya kumtimua Gachagua ili tupambane nayo bunge, lakini kumbuka kuwa kabla ya kuileta, sharti maoni ya wananchi yashirikishwe kutoka kaunti moja hadi nyingine.”

Profesa Macharia Munene anasema kuwa kuanzia siku ya kuapishwa kwake, Naibu Rais amekuwa akifanya makosa.

“Ikiwa Gavana Mutahi Kahiga wa Nyeri anasema kweli, je, ni Ruto alimwambia azungumze kuhusu hisa. Kwa hivyo, Gachagua alipoongea kuhusu hisa hakuelewa hali halisi ya uongozi nchini Kenya. Hili ni kosa la kwanza ambalo Naibu Rais alitenda,” akasema Profesa Munene, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU).

Msomi huyo anasema kuwa misukosuko inayoshuhudiwa ndani ya serikali ya Kenya Kwanza wakati huu ilibashiriwa kutokea.

“Yote yanafanyika serikalini sasa yalitarajiwa. Huku akileweshwa na tamaa ya kutaka akubalike kama kiongozi wa Mlima Kenya, hakutaka kuwasikia wale waliomwonya kuhusu kile ambacho kingemtendekea.“Japo anafanya kazi nzuri ya kuonyesha kuwa anadhulumiwa ili Wakenya wamhurumie, huenda huruma hizo zikawa za muda mfupi tu,” anaongeza Profesa Munene.