Habari za Kitaifa

NPSC sasa kuajiri makurutu 10,000 wa polisi mwaka huu

Na  ANTHONY KITIMO September 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Tume ya Huduma kwa Polisi (NPSC), imetangaza kuanza kwa mchakato wa kuajiri makurutu wapya 10,000, ikiwa ni hatua ya kwanza tangu tume hiyo iundwe kikamilifu.

Akizungumza katika kikao rasmi cha kwanza cha tume hiyo, Mwenyekiti wa Tume, Dkt Amani Komora, alisema kuwa lengo la hatua hiyo ni kuongeza nguvu kazi ya polisi ili kukidhi mahitaji ya kiusalama yanayoendelea kubadilika kote nchini.

“Pamoja na Inspekta Jenerali Douglas Kanja, na kwa uwezo wangu kama mwenyekiti, naunga mkono uamuzi wa tume kuanzisha mchakato wa kuajiri makurutu 10,000. Hatua hii imejiri wakati muhimu ambapo idadi ya maafisa wa polisi inapungua kutokana na sababu kama vile kustaafu kwa kawaida na nyinginezo,” alisema Dkt Komora.

Alieleza kuwa masuala ya maslahi ya maafisa, ikiwemo mishahara ya polisi, yatashughulikiwa katika mikutano ijayo.

Dkt Komora aliahidi kumaliza migongano ya ndani ya tume hiyo ili kuhakikisha huduma ya polisi inaimarishwa na kuwa na maafisa wa kutosha.

“Tumekubaliana kuhusu kugawana majukumu kwa makusudi ili kuwe na uratibu mzuri. Tumetengeneza mpango wa mchakato wa ajira itakayowezesha uwazi katika huduma,” aliongeza.

Tangazo hilo lilitolewa katika Shule ya Serikali ya Kenya mjini Mombasa, ambako makamishna walihudhuria kikao cha mafunzo. Katika kikao hicho, Profesa Colette Suda alichaguliwa kuwa Naibu Mwenyekiti wa Tume.

Kuhusu suala la mishahara ya maafisa wa polisi, Dkt Komora aliwataka Wakenya kuwa na subira huku tume ikifanya kazi kutatua changamoto iliyopo.

“Tumeshughulikia masuala mengi na kugawana majukumu. Suala la mishahara litajadiliwa katika mikutano ijayo,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Sasa kwa kuwa tume imekamilika kikamilifu, tuna imani kuwa tutaongoza mageuzi makubwa yatakayoweka msingi wa huduma ya polisi iliyobobea, inayoitikia mahitaji ya watu na inayoendeshwa kitaalamu.”

Makamishna wote, akiwemo Inspekta Jenerali Douglas Kanja na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Mohammed Amin, walihudhuria kikao hicho cha mafunzo.