Habari za Kitaifa

Nuru Okanga motoni kwa matamshi ya uchochezi

June 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Milimani imeamuru mwanaharakati wa kisiasa Nuru Maloba Okanga azuiliwe kwa siku tano kuhojiwa na kuchunguzwa kutokana na matamshi ya uchochezi kuhusu uhusiano wa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Rais William Ruto.

Hakimu mwandamizi Ben Mark Ekhubi aliagiza Okanga azuiliwe katika kituo cha polisi cha Muthaiga kuhojiwa na maafisa wa idara ya uchunguzi wa jinai (DCI).

Akiwasilisha ombi la kuzuiliwa kwa Okanga kiongozi wa mashtaka Virginia Kariuki alieleza mahakama kwamba maafisa kutoka kitengo cha uchunguzi wa uhalifu wanahitaji muda kuchunguza matamshi yanayozua utata katika mitandao ya kijamii.

Bi Kariuki alisema mwanaharakati huyo ambaye ni mfuasi sugu wa muungano wa Azimio amenukuliwa katika mtandao wa Tittok akieneza maneno ya uchochezi ambayo yanaweza kuzua mtafaruku wa kijamii.

Hakimu alielezwa maafisa wa DCI katika kitengo cha uhalifu wa kimitandao wanachunguza matamshi ya Okanga akimshauri Bw Gachagua amsumbue mno Rais Ruto.

Katika ukanda wa video unaosambazwa katika mitandao ya kijamii, polisi wamesema Okanga amerekodiwa akimtaka naibu rais awe na msimamo mkali na kumtesa na kumsumbua Rais Ruto.

Mahakama ilielezwa katika ukanda huo Bw Okanga amenukuliwa akisema Bw Gachagua alikuwa Afisa wa Utawala aliyefundishwa jinsi ya kutumia silaha.

Bi Kariuki alisema Okanga alinukuliwa akisema Bw Gachagua anatakiwa kujihami na bastola kisha amdhuru Dkt Ruto.

“Maafisa wa DCI wanahitaji muda wa siku 21 kumhoji Okanga kisha waandike taarifa kutoka kwa mashahidi kuhusiana na matamshi ya uchochezi yanayozua taharuki miongoni mwa wananchi,” Bi Kariuki alimweleza hakimu huku akiomba mshukiwa “azuiliwe kuhojiwa kabla ya kufunguliwa mashtaka.”

Mahakama ilielezwa kwamba baada ya uchunguzi kukamilishwa, mshukiwa huyu atafunguliwa mashtaka ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii kwa nia ya kutekeleza ‘uhalifu’.

Mawakili wake, Shadrack Wambui na Kevin Onani walipinga vikali ombi hilo la kumzuia mshukiwa kwa siku 21.

Waliomba Okanga aachiliwe kwa dhamana wakisema “hawezi kuzuia polisi kutoka kitengo cha DCI kusikiza kanda za video katika afisi zao.”

Bw Wambui alieleza mahakama mshtakiwa hawezi kuvuruga polisi wakichunguza kesi hiyo.

“Mashahidi wakuu katika kesi hii ni maafisa wa polisi na Okanga hawezi kuvuruga maafisa wa usalama wakiendelea na kazi yao. Mwachilie kwa dhamana na kumuonya asiingilie uchunguzi,” Bw Wambui alisema.

Wakili huyo alieleza mahakama mshtakiwa atatii masharti ya dhamana.

Bw Ekhubi aliamuru Okanda arudishwe tena kortini Juni 17, 2024.