Nyong’o akosoa amri ya kufutwa kwa wafanyakazi wa viwanda vya sukari
GAVANA wa Kisumu, Profesa Anyang’ Nyong’o, amekosoa vikali hatua ya Katibu wa Wizara ya Kilimo Kipronoh Ronoh kuidhinisha kufutwa kazi kwa maelfu ya wafanyakazi katika viwanda vya sukari vinavyomilikiwa na serikali.
Prof Nyong’o ametaja uamuzi huo kama wa kikatili, usiozingatia maslahi ya wananchi na usaliti kwa juhudi za kufufua sekta ya miwa ambazo zimekuwa zikiendelezwa nchini.
“Uamuzi huu sio tu wa kusikitisha bali ni hatari kwa ustawi wa sekta ya miwa. Tulikubaliana kuwa shabaha ya kukodisha viwanda hivyo ni kufufua uzalishaji na kuboresha maisha ya wakulima na wafanyakazi si kuwakeketa,” alisema Nyong’o.
Katibu Ronoh ameagiza wakurugenzi wakuu wa viwanda vya Sony, Chemelil, Muhoroni na Nzoia kuarifu wafanyakazi wote kwamba mikataba yao ya ajira itasitishwa, hatua ambayo itaathiri zaidi ya wafanyakazi 5,000.
Prof Nyong’o aliongeza kuwa hatua hiyo ni kinyume na lengo la serikali la kufufua sekta ya sukari kupitia ukodishaji wa viwanda kwa sekta ya binafsi kuongeza ufanisi na kuimarisha maisha ya wahusika wote.
“Kupitisha maamuzi ya kufuta kazi wafanyakazi kabla ya kulipwa kwa madeni wanayodai ni kinyume na haki na maadili. Hii ni kama kumwagia chumvi jeraha,” alisema kwa hasira.
Gavana huyo pia alilalamikia kukosekana kwa mashauriano kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti zinazohusika, akisema kuwa maamuzi yanayoathiri uchumi wa kaunti kadhaa yalifanywa bila kushirikisha uongozi wa eneo.
“Hili ni kinyume na maadili ya utawala wa pamoja kama ilivyoainishwa katika Katiba. Sekta ya sukari ni jukumu lililogatuliwa, hivyo maamuzi hayawezi kufanywa kwa siri kutoka ofisini Nairobi,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Gavana Nyong’o, serikali kuu iliahidi kulipa madeni ya wafanyakazi wa zamani wa viwanda hivyo, na ni kinyume cha haki kuwafuta kazi kabla ya kutimiza ahadi hiyo.