Habari za Kitaifa

Nyumba ya mpiganiaji uhuru yabomolewa Kariobangi

January 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA STEVE OTIENO

MAMIA ya wakazi wa mtaa wa Kariobangi South KCC katika barabara ya Kangundo, usiku wa kuamkia Jumatano walikesha kwenye baridi baada ya jengo la ghorofa tatu wanakoishi kubomolewa.

Jengo hilo lililokuwa makazi ya zaidi ya familia 50 lilibomolewa na kuchangia kupotea kwa mali ya mamilioni ya pesa. Zaidi ya vijana 100 ambao walikuwa wamejihami kwa fimbo na mawe, waliwatimua wakazi walioamshwa usingizi saa nane usiku wa kuamkia Jumatano.

Mwanzoni walifikiria walikuwa wamevamiwa na kundi la wezi ambalo lilikuwa likitaka kupora mali yao lakini wakashangaa zaidi tingatinga lilipowasili na kuanza kuangusha jengo hilo.

“Kila kitu ambacho nilikuwa nacho kimepotea hapa. Sijui mwelekeo ambao nitauchukua. Kwa nini mtu apange unyama huu dhidi ya maskini katika nchi hii?” akahoji Jamila Molu, ambaye alikesha na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili kwenye kijibaridi kikali.

Jengo hilo linamilikiwa na Miriam Bilali na Mwanaisha Bilali, wajukuu wa Mwanaisha Bilali, shujaa wa Maumau ambaye alifahamika kama Mama Uhuru.

Mwanaisha Chebet Bilali, mmiliki wa nyumba ya ghorofa iliyobomolewa na serikali ya Kaunti ya Nairobi kupisha soko la Kangundo mnamo Januari 10, 2024. PICHA | BILLY OGADA

Bi Mwanaisha alisema kuwa walikabidhiwa kipande hicho cha ardhi ambapo walijenga jumba hilo mnamo 2002 na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, wakati huo akiwa waziri wa serikali za mitaa.

Familia hiyo ilipewa ardhi hiyo Januari 7, 2002 baada ya kutimiza masharti yaliyokuwa yakitakikana ikiwemo kulipa ada ya Sh10,000 na kodi ya ardhi ya Sh2,080.

Familia ya mpiganiaji huyo wa uhuru ilipewa ardhi hiyo miaka michache baada ya kupewa nyumba eneo la Pumwani miaka ya 90. Kuna hata cheti kinachoonyesha Bw Kenyatta akimpa marehemu shujaa huyo wa uhuru cheti cha kumiliki nyumba Pumwani.

Hata hivyo, maji yalianza kuzidi unga mnamo 2021 baada ya usimamizi wa jiji (NMS) kuwaamrisha wahame kipande hicho cha ardhi walichopewa na serikali.

Familia hiyo ilielekea mahakamani na kupata amri ya kuzuia jengo lao kubomolewa na ardhi kutwaliwa.

Hakimu Mkuu Mkaazi M.W Murage alitoa uamuzi mnamo Septemba 27, 2021, wa kuzuia ubomozi huo na inashangaza kuwa ulitekelezwa licha ya amri ya korti.

Kamanda wa Polisi wa Nairobi Adamson Bungei alisema ubomoaji huo ulitekelezwa na kaunti ambayo inadai ardhi hiyo.

“Kaunti inasema jengo lipo katika ardhi yake ambayo pia ipo soko la Kangundo na wanataka kuitwaa. Polisi hawakuhusika na suala hili na baada tu ya familia kuwasilisha malalamishi yao, tutachunguza suala hili,” akasema Bw Bungei.