Habari za Kitaifa

‘Obado alikuwa kwa Raila usiku ule Sharon aliuawa’

May 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Gavana wa Migori Okoth Obado alikuwa katika makazi ya kinara wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga mtaani Karen usiku ule mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo Sharon Otieno aliuawa Septemba 2018, Mahakama Kuu imeelezwa.

Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Cecilia Githua anayesikiliza kesi ya mauaji ya Sharon dhidi ya Obado, afisa wa polisi aliyechunguza kesi hiyo, Bw Nicholas ole Sena, alithibitisha kwamba Bw Obado alikuwa katika makazi ya Bw Odinga.

“Bw Obado alikuwa katika makazi ya Bw Odinga mtaani Karen usiku ule Sharon aliuawa. Bw Obado hakuwa katika Kaunti ya Homa Bay ila alikuwa Nairobi usiku wa Septemba 3 na Septemba 4, 2018, Sharon alipouawa,” Bw Ole Sena alimweleza Jaji Githua.

Bw Obado ameshtakiwa pamoja na aliyekuwa msaidizi wake Bw Michael Oyamo na mfanyakazi katika serikali ya Kaunti ya Migori Bw Caspal Obiero kwa mauaji ya Sharon.

Sharon alikuwa na umri wa miaka 26 alipokumbana na mauti.

Waliomuua walimdunga na chuma kwenye tumbo na kusukuma ikatokezea kwenye mgongo.

Aliaga dunia pamoja na mtoto tumboni kwa sababu alikuwa na mimba ya miezi saba.

Uchunguzi wa DNA ulibaini kwamba mimba ya Sharon ilikuwa ya Bw Obado.

Sharon na mwanaye waliuawa katika eneo la Owade, Rachuonyo, Kaunti ya Homa Bay.

Mwanafunzi huyo aliuawa pindi baada ya kutekwa nyara na mwanahabari aliyetoroka na kumwacha Sharon mikononi mwa wauaji.

Jaji Githua alielezwa kwamba Bw Obado alikuwa katika makazi ya Bw Odinga kati ya saa kumi na moja alasiri hadi saa tatu usiku.

Bw Ole Sena alieleza mahakama kwamba uchunguzi ulibaini kwamba Bw Obado alikuwa Nairobi kati ya Septemba 2 hadi Septemba 5, 2018.

“Nathibitisha kwamba Bw Obado alikuwa Nairobi,” Bw Ole Sena alisema alipohojiwa na wakili Kioko Kilukumi anayemwakilisha Bw Obado.

Mchunguzi huyo wa masuala ya jinai alisema “hakuna ushahidi wa kumhusisha Bw Obado na utekaji nyara wa Sharon siku ile alipouawa.”

“Eleza hii mahakama sababu ya kumshtaki Bw Obado na mauaji ya Sharon,” Bw Kilukumi alimwelekezea afisa huyo.

“Bw Obado alishtakiwa kwa mauaji ya Sharon kwa sababu ndiye alikuwa amemweka mimba,” Bw Ole Sena alijibu.

Alipohojiwa zaidi, Bw Ole Sena alisema sio makosa Bw Obado kumtia mimba Sharon kwa vile mwanafunzi huyo alikuwa mtu aliyekuwa amekomaa kubeba mimba.

“Kwa hakika Bw Obado alikuwa amejitolea kugharimia malezi ya mtoto huyo. Alikuwa pia amejitolea kumnunulia nyumba Sharon jijini Nairobi waishi na mwanawe,” Bw Ole Sena alieleza Jaji Githua.

Bw Obado alifikishwa kortini Septemba 24, 2018, na kushtakiwa kwa mauaji ya Sharon.

Alikaa rumande kwa miezi kadhaa kabla ya kuachiliwa kwa dhamana.

Kufikia sasa, mashahidi 42 wametoa ushuhuda wao.

Upande wa mashtaka unaoongozwa na naibu mkurugenzi wa mashtaka ya umma Gikui Gichuhi, uko karibu kukamilisha kesi hiyo.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa.