• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Obasanjo afichua alicheza chini ya maji kuzima maandamano ya Azimio

Obasanjo afichua alicheza chini ya maji kuzima maandamano ya Azimio

JUSTUS OCHIENG Na CHARLES WASONGA

KWA mara ya kwanza baada ya zaidi ya miezi saba, aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo ametoboa kuwa aliongoza mazungumzo kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga, hatua iliyositisha maandamano dhidi ya serikali.

Bw Obasanjo ambaye mnamo Februari 15, 2024, alimpendekeza Bw Odinga kwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), alisema alipatanisha wawili hao Julai 29, 2023, ndani ya mkahawa mmoja katika jiji la Mombasa.

Bw Obasanjo alielezea furaha yake kwamba Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco) ilifanya kazi nzuri.

Baadaye kiongozi huyo anayeheshimiwa barani Afrika alikutana na Rais Ruto mjini Murang’a ambako kiongozi wa taifa alikuwa huko katika ziara ya kikazi. Alifanya hivyo muda mfupi baada ya kuhutubia wanahabari jijini Nairobi akiwa pamoja na Bw Odinga.

“Miezi kadha iliyopita nilikuwa hapa Kenya ambapo nilikutana na Rais Ruto na Bw Odinga na tukaenda Mombasa na matokeo yake yakawa matokeo ya shughuli hiyo iliyoendesha na wanachama watano kutoka kila mmojawapo wa mirengo hiyo miwili iliyounda kamati hiyo,” Bw Obasanjo akasema akirejelea kamati ya Nadco iliyoongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah (kwa niaba ya mrengo wa Kenya Kwanza) na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa niaba ya Azimio.

Wanachama wengine wa upande wa Kenya Kwanza walikuwa ni Gavana wa Embu Cecily Mbarire, Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar na Mbunge Mwakilishi wa Kike Bungoma Catherine Wambilianga.

Wawakilishi kutoka mrengo wa Azimio walikuwa Kiongozi wa Wachache Opiyo Wandayi, kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa, Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni na Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi.

Mnamo Alhamisi Bw Obasanjo alifichua kuwa alifahamishwa kwamba timu hiyo ilifanya kazi nzuri.

“Kamati hiyo ilifanya kazi nzuri. Tunaamini kuwa ukizima moto sharti uhakikishe umedhibitiwa kabisa,” Bw Obasanjo akasema.

Awali kabla ya ufichuzi wake, ilikuwa imedaiwa kuwa Rais huyo wa zamani wa Nigeria alipatanisha Rais Ruto na Bw Odinga jijini Mombasa, suala hilo lilikuwa limebakia uvumi tu.

Ni kwa sababu alichelea kupiga picha ya pamoja na viongozi hao wawili. Lakini iliaminika kuwa alitumwa na jamii ya kimataifa kuzima mzozo huo wa kisiasa.

Uungwaji wa Bw Odinga kuwa mwenyekiti wa AUC kurithi Moussa Faki unadhihirisha Bw Obasanjo alisuka mambo chini ya maji.

Mnamo Ijumaa viongozi wa Azimio wakiongozwa na Bw Musyoka walitoa taarifa wakisema wanaunga mkono azma ya kinara wao.

Mnamo Jumamosi, chama cha Rais Ruto–United Democratic Alliance (UDA)–kilitangaza kwamba kinamuunga mkono Bw Odinga kuendea nafasi ya mwenyekiti AUC.

Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala alisema Bw Odinga ana tajriba pevu kwa wadhifa huo.

“Bw Odinga ni mwanauanamajumui wa Afrika ambaye kwa miaka mingi amejitolea kwa ustawi wa Waafrika. Anaelewa changamoto zinazolikumba bara hili ambazo ni pamoja na ukoloni mamboleo, vita dhidi ya kukaliwa na baadhi ya mataifa ya kigeni na udikteta wa baadhi ya viongozi wa Afrika,” akasema Bw Malala.

Aliongeza kwamba Bw Odinga alionyesha ujasiri mkuu kwa kukabiliana na maadui wa demokrasia.

Lakini huku Bw Obasanjo akipongeza kazi wa Nadco ambayo ripoti yake sasa imewasilishwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti ijadiliwe, kundi la wabunge wa Kenya Kwanza walifichua wiki jana kuwa ripoti hiyo inatumiwa kama chambo cha kumshurutisha Bw Odinga kuunga mkono sera tata ya utozaji ushuru tata wa Nyumba.

  • Tags

You can share this post!

Msanii Nyashinski ateswa na kesi mahakamani

Meneja wa duka ashtakiwa kuiba bidhaa za mifugo za thamani...

T L