Oburu aanza hatamu ya uongozi ODM baada ya kuwa chini ya kivuli cha Raila miaka mingi
SENETA wa Siaya Dkt Oburu Oginga leo Oktoba 27, 2025 anaanza kazi rasmi kama kaimu kiongozi wa ODM huku malumbano ya ndani kwa ndani yakitishia kusambaratisha chama hicho baada ya kifo cha Raila Odinga.
Dkt Oginga ataandaa mkutano wa Kamati Kuu ya chama ambao unatarajiwa kurasmisha nafasi yake kama kiongozi wa chama baada ya kifo cha Raila mnamo Oktoba 15.
Kwa miaka mingi seneta huyo alikuwa uongozini chini ya kivuli cha Raila na anachukua usukani wakati maasi na malumbano yameanza kushuhudiwa ndani ya ODM.
Kiazi moto kwa Dkt Oginga ni tofauti kati ya viongozi iwapo ODM inastahili kuendelea kushirikiana na utawala wa Rais William Ruto au la baada ya kifo cha Raila.
Akiwa na umri wa miaka 82, pia Dkt Oginga ana kazi kuhakikisha ODM inadumisha umaarufu na sura yake ya kitaifa jinsi ilivyokuwa wakati wa Raila.
Viongozi waasi ndani ya ODM wanaongozwa ni Katibu Mkuu Edwin Sifuna, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na mwenzake wa Saboti Caleb Amisi.
Dkt Oginga mwenyewe amenukuliwa akisema kuwa anaunga mkono Serikali Jumuishi akisisitiza kuwa kabla ya mauti yake Raila alikuwa ndani ya serikali.
Bw Sifuna na kundi lake hata wakati ambapo Raila alikuwa hai, alikuwa ametishia kuondoka ODM iwapo chama hicho kitaunga mkono Rais Ruto kutwaa mamlaka kwa muhula wa pili.
Licha ya kuwa alikuwa akiunga Serikali Jumuishi, Raila mwenyewe alikuwa mstari wa mbele kuwatetea wanasiasa waasi baada ya baadhi ya wandani wake kutishia kuwafurusha chamani.
Mkutano wa leo unalenga kuangazia jinsi ambavyo chama kitaendelea na shughuli zake kikijiandaa kwa uchaguzi wa 2027.
Kwa mujibu wa Dennis Onyango ambaye alikuwa Msemaji wa Raila, mkutano wa leo ni wa kawaida na utazungumzia jinsi maisha yatakavyoendelea baada ya mauti ya Raila.
“Si mkutano wa dharura na utazungumzia maadhimisho ya miaka 20 ya ODM na pia kuwa mikutano ya kumuenzi Raila iandaliwe sehemu nyingine za nchi,” akasema Bw Onyango.
“Pia utazungumzia jinsi chama kilishughulikia kifo cha Raila na kwa sababu tuna kiongozi mpya, naye lazima ajifahamishe na ngazi mbalimbali ya chama pamoja na walio chini yake. Mkutano huu unaonyesha kuwa msingi ambao Raila aliuacha nao ODM bado ni imara,” akaongeza.
Taifa Leo imebaini kuwa Dkt Oginga aliteuliwa kaimu kiongozi wa ODM na wanasiasa ambao hawakumtaka Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o achukue wadhifa huo.
Wakati ambapo Raila alikuwa akiwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), aliachia Profesa Nyong’o uongozi wa ODM.
Profesa Nyong’o na Gavana wa Siaya James Orengo hawakuwa wakishabikia sana Serikali Jumuishi. Wawili hao pia hawashikilii wadhifa wowote katika uongozi wa ODM na hilo linafanya iwe rahisi kupigwa kumbo kuhusu masuala ya chama na siasa za urithi wa nafasi ya Raila.
Dkt Oginga mwenyewe wiki jana alipuuzilia mbali taharuki zinazotokana na pengo ambalo aliliacha Raila akisema kuwa kiongozi kigogo wa jamii ya Waluo na hata wa ODM atajitokeza tu mwenyewe baada ya muda.
“Wengine wamekuwa wakiuliza jinsi ambavyo nitaongoza chama katika umri wangu. Niliwaambia kuwa kiongozi yeyote ana uwezo wa kuongoza ODM,” akasema Dkt Oginga.
Aliongeza kuwa hata Raila mwenyewe hakuteuliwa kuongoza jamii ya Waluo lakini alitumia nguvu na ujanja wake kisiasa kujikweza ngazi na hadhi.
Naibu Kiongozi wa ODM Godfrey Osotsi naye alisema mkutano wa leo hautakuwa na ajenda kubwa kwa sababu wanachama bado wanaomboleza kifo cha Raila.
“Tutamakinikia umoja wa chama na chaguzi ndogo zinazokuja mwezi ujao,” akasema Bw Osotsi.
ODM imepanga kuandaa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe mnamo Machi mwaka ujao ambapo viongozi wa chama watachaguliwa.
Kongamano hilo lilistahili kuandaliwa Oktoba hii lakini likaahirishwa ili kutoa nafasi kwa chama kuendelea na sherehe za kuadhimisha miaka 20 tangu ODM ianzishwe.