Habari za Kitaifa

Oburu aita mkutano ODM shinikizo za kumtaka aachilie kiti zikizidi

Na COLLINS OMULO, KEVIN CHERUIYOT January 12th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

VITA vikali vinavyoendelea kushuhudiwa ndani ya ODM vimekilazimisha chama hicho kuandaa mkutano wa dharura leo huku wanasiasa kadhaa wakimtaka Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga abanduliwe kama kiongozi wa chama hicho.

Kamati Kuu (CMC) ya ODM, ambayo ndiyo ya juu zaidi katika kufanya maamuzi ya chama, itaandaa mkutano wake leo katika Kaunti ya Kilifi.

Mkutano huo unatarajiwa kutuliza au kupandisha joto zaidi chamani hasa suala la uchaguzi mkuu wa 2027 likitarajiwa kujadiliwa.

Pia kikao hicho kinajiri baada ya baadhi ya wanachama wa ODM kutaka Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) liandaliwe, wakizua maswali kuhusu iwapo Dkt Oginga yuko uongozini kihalali.

Ushirikiano wa ODM na utawala wa Rais William Ruto umezua majibizano makali kati ya Katibu Mkuu Edwin Sifuna na Kiongozi wa Wachache Junnet Mohamed.

Madai yamezuka kuwa baadhi ya wanasiasa wanajaribu kuuza ODM. Pia kuna majibizano makali kuhusu nani anastahili kulaumiwa kuhusu Raila Odinga kukosa ushindi kwenye uchaguzi wa 2022.

Seneta wa Migori Eddy Oketch wiki jana alitekeleza vitisho vya kumtimua Seneta Sifuna kwenye kamati zote za seneti na pia afurushwe chamani akidai amekuwa akitoa matamshi yanayoenda kinyume na msimamo wa ODM.

Hata hivyo, jaribio hilo lake lilizimwa na Mama Ida Odinga na Dkt Oginga.

Vikao vya CMC huongozwa na kiongozi wa ODM na hushughulikia utatuzi wa mizozo inayotokea ndani ya chama.

Wanachama wake ni kiongozi wa chama, mwenyekiti, katibu, katibu mtendaji, mkurugenzi wa uchaguzi, viongozi wa vijana na wanawake, wanachama watatu walioteuliwa na kiongozi wa chama pamoja na mkurugenzi mkuu wa chama.

Ajenda kuu ya leo ni ushirikiano ndani ya Serikali Jumuishi na mikakati ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Pia kutakuwa na majadiliano kuhusu lini NDC itaandaliwa.

Ingawa hivyo, mkutano huo umezua cheche kali, Naibu Kiongozi wa ODM Godfrey Osotsi akisema aliomba uahirishwe ili wanachama wa kamati zote wahudhurie lakini pendekezo lake halikutiliwa maanani.

“Niko nje ya nchi kwa shughuli za seneti na niliomba kiongozi wa chama aahirishe mkutano huo lakini ni kama ombi langu lilipuuzwa,” akasema Bw Osotsi ambaye pia ni Seneta wa Vihiga.

Baada ya kifo cha Raila, uthabiti wa miaka 20 wa ODM unaonekana kuwa hatarini.

Tofauti kuhusu ushirikiano ndani ya Serikali Jumuishi, uhalali wa Dkt Oginga kama kiongozi wa chama na kuandaliwa kwa NDC vinatishia kusambaratisha ODM.

Mbunge wa Embakasi Babu Owino anasema wakati umefika ambapo viongozi chipukizi wanastahili kutwaa uongozi wa ODM, kauli ambayo imefasiriwa kuwa ya kupinga uongozi wa Dkt Oginga.

Baadhi ya viongozi wa Pwani nao wanamtaka Waziri wa Madini, Hassan Joho awe kiongozi wa chama iwapo NDC itaandaliwa.

Hii ni licha ya Baraza Kuu la Uongozi wa ODM kuidhinisha Dkt Oginga kama kiongozi wa chama miezi miwili iliyopita baada ya kuwa kaimu kiongozi tangu Oktoba 15 Raila alipokufa.

Pwani imeunga ODM na Joho amewekeza sana ndani ya chama. Huu ndio wakati wa kuhakikisha uongozi wa chama unamwendea Joho,” akasema Waziri wa zamani wa Jinsia Aisha Jumwa.

Dkt Oginga naye akiwajibu wanaotilia shaka uongozi wake, alisema yuko tayari kuitisha NDC akisema hawaogopi wakosoaji wake.

“Wale wanaozua maswali kuhusu uchaguzi wangu, nawaambia waje NDC kwa sababu siogopi na nitaitisha kongamano hili hivi karibuni. Mimi ndiye nilikuwa nahudhuria mikutano yote ya Serikali Jumuishi kama mwenyekiti wakati Raila alikuwa hai na hakuna kitu nisichokijua,” akasema Dkt Oginga akishikilia anatosha kuongoza chama baada ya kifo cha Raila.

Alikuwa akizungumza kwenye mazishi Kaunti ya Siaya wikendi ambapo Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi aliapa kuwa watazima juhudi zozote za kumbandua Dkt Oginga kwenye uongozi wa ODM.

“Yeyote anayelenga kumwondoa Oburu anaota ndoto za mchana,” akasema.

Mbunge wa Makadara George Aladwa naye ameshutumu mkutano wa baadhi ya wabunge na viongozi wa ODM wiki jana ambapo wito wa kumngóa Dkt Oginga ulizungumziwa.