Habari za Kitaifa

ODM sasa yakohoa na kuonya Ruto kuhusu utekaji nyara

Na JUSTUS OCHIENG December 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga kimetoa onyo kali, kikitishia kuongoza maasi ya raia dhidi ya utawala wa Rais William Ruto kutokana na kile kinachosema ni kuibuka kwa siasa za kidikteta na dhuluma.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, kiongozi wa muda wa chama hicho, Prof Anyang’ Nyong’o, ambaye ni Gavana wa Kisumu alikosoa visa vya utekaji nyara vinavyoendelea kote nchini akisema watapinga majaribio ya serikali ya kuwakandamiza Wakenya.

“Tuko tayari kuongoza maasi dhidi ya siasa za kidikteta na dhuluma ambazo zinajaribu kulazimisha utawala dhalimu na usio wa kidemokrasia kwa watu kupitia mambo kama vile utekaji nyara na vitisho vya kisiasa,” Prof Nyong’o alisema.

Aliendelea: “Kwa hivyo tunaionya sana serikali ikomeshe utekaji nyara huu wa woga wa wale wanaokosoa sera zisizo za kidemokrasia.”

Bw Odinga awali alikuwa ameonya kwamba Wakenya hawawezi kuvumilia utekaji nyara akitaja kama ujambazi.

Bw Odinga alitaka kukomeshwa kwa utekaji nyara ambao ulisababisha maandamano nchini kote Jumatatu.

“Haya ni matukio hatari sana. Ni kama serikali ya utawala wa mafia ambapo watu wanaofanana na maafisa wa polisi huwateka nyara Wakenya mchana peupe.

“Wanafanana na genge la jenerali Papa Doc Duvalier na kikosi chake cha wanamgambo wa Tonton Macoute ambao walikuwa wakiteka nyara watu na kuwatesa. Kwa hivyo, huu ni kama ujambazi na si jambo ambalo tunaweza kuvumilia katika nchi yetu,” alisema.

Katika mahojiano yake na Taifa Leo, Prof Nyong’o alibainisha kuwa kushiriki kwa chama cha ODM katika serikali jumuishi hakufai kuchukuliwa kumaanisha kukumbatia sera za “kandamizi”.

“Tunajua mustakabali wetu kama chama. Lakini hatuwezi kutabiri mustakabali wa siasa. Tulicho na uhakika nacho katika siku zijazo ni dhamira yetu kama chama cha kitaifa cha demokrasia na mageuzi.

“Kuwa wanamageuzi hakumaanishi kuchukua silaha na kupigania mabadiliko. La hasha. Tunamaanisha kuwa tayari kuongoza maasi ya wananchi dhidi ya siasa za kidikteta na kandamizi,” akasema.

Prof Nyong’o pia aliangazia mipango ya muungano wa chama na azma ya Bw Odinga kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA