Habari za Kitaifa

ODM yadai Ruto anadhoofisha chama chao kutoka ndani

Na JUSTUS OCHIENG, MOSES NYAMORI January 9th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

MAPAMBANO mapya ya kisiasa yameibuka ndani ya Serikali Jumuishi, baada ya kundi la viongozi wa chama cha ODM kudai kuwa Rais William Ruto anatumia wanachama wa ‘Chungwa’ katika vikosi vya kikanda anavyounda akiwa na lengo la kukidhoofisha chama hicho.

Wakiongozwa na Naibu Kiongozi wa ODM, Godfrey Osotsi, viongozi hao wanadai kuwa kuna mkakati wa kisiasa uliopangwa vyema kudhoofisha chama hicho kutoka ndani, kwa kuwahusisha wabunge wa ODM katika mipango ya mapema ya kampeni ya Rais Ruto ya kutafuta muhula wa pili.

Bw Osotsi alisema hatua hiyo ni juhudi za kuondoa mizizi ya ODM mashinani na kutumia mitandao ya chama kwa maslahi ya kampeni zake za uchaguzi mkuu wa 2027.

Kiini cha mvutano huo ni eneo la Magharibi mwa Kenya, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likibadilika-badilika kisiasa, na sasa linaibuka kama kitovu muhimu cha mapambano ya kisiasa kufuatia kukosekana kwa ushawishi wa Raila Odinga.

Viongozi wa ODM wanasema kinachoendelea ni “uvamizi wa kisiasa” ulioratibiwa kwa lengo la kudhoofisha chama hicho, huku Rais akiunda vikosi vya kikanda vya kampeni vinavyojumuisha wabunge wa ODM.

Bw Osotsi alitoa madai hayo katika taarifa jana ambapo alishutumu UDA kwa kutumia Serikali Jumuishi kupenya ngome za ODM.

Kulingana na Bw Osotsi, kisa cha hivi karibuni ni kikao cha Januari 6 katika Hoteli ya Golf mjini Kakamega, ambapo wabunge na maafisa kadhaa waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM walihudhuria vikao vya mikakati vilivyoitishwa na viongozi wakuu wa UDA.

“Wabunge na maafisa wa ODM katika kaunti za Vihiga na Kakamega wamejumuishwa katika mikutano ya mikakati ya uchaguzi na kampeni ya UDA,” alisema Bw Osotsi, akieleza kuwa hatua hiyo inakiuka Sheria ya Vyama vya Kisiasa na katiba ya ODM.

Alidai kuwa wanachama wa ODM wameshirikishwa katika chaguzi za nyanjani za UDA kwa madai ya uongo kuwa ODM na UDA zina makubaliano rasmi ya ushirikiano hadi ngazi ya mashinani.

Viongozi wa chama wanasisitiza kuwa ajenda ya mageuzi ya vipengele 10 iliyotiwa saini Machi 2025 kati ya ODM na UDA, haikulenga kuanzisha shughuli za pamoja za uchaguzi.

“Ajenda ya mageuzi, kama serikali jumuishi yenyewe, ni ya muda na inapaswa kuisha 2027,” alisema Bw Osotsi.

“Haiwezi kutafsiriwa kama mkataba wa ushirikiano wa kisiasa kati ya ODM na UDA.”

Kwa mtazamo wake, mkakati wa UDA ni kutumia mitandao ya mashinani ya ODM iliyojengwa kwa zaidi ya miaka 20 kuvamia Magharibi mwa Kenya, kuwatenga viongozi wanaopinga ushirikiano baada ya 2027 na hatimaye kukidhoofisha chama bila kuzua hasira za wananchi.

Wachambuzi wa siasa wanasema bila Raila, eneo la Magharibi sasa ni wazi kwa ushawishi wa vyama mbalimbali, hali ambayo Rais Ruto anaonekana kulenga kwa makusudi.

“Magharibi, bila Raila, sasa ni uwanja ulio wazi, na hilo ndilo Rais Ruto anatumia,” alisema mchambuzi wa siasa Dismas Mokua.

Jumanne, Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Ford–Kenya, pamoja na Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula, waliongoza mkutano mjini Kakamega, wakafanya kampeni ya wazi ya muhula wa pili wa Rais Ruto mwaka 2027.

Wabunge kadhaa, wakiwemo waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM, walihudhuria.

Kundi hilo linaloongozwa na Gavana Lusaka ni sehemu tu ya mpango wa kuunda upya muundo wa kampeni ya Rais Ruto.

Duru zinasema vikosi vya kikanda vinaendelea kuundwa kimya kimya katika maeneo ya Nyanza, Mashariki, Pwani na Nairobi.

Nchini Nyanza, viongozi wanaounga mkono serikali jumuishi wamekuwa wakizunguka maeneo ya Luo Nyanza wakihimiza huko Pwani, mpango huo umemekuwa ukiendelea kwa kivuli cha vikao vya maendeleo na michango ya harambee.

“Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ya 81 ya Raila Odinga yaliyofanyika Kilifi Jumatano, viongozi kadhaa walizungumza kwa hisia kuhusu ‘kujitoa kwa muda mrefu’ kwa Waziri wa Madini, Hassan Joho, ndani ya chama, wakisisitiza kuwa juhudi zake zinafaa kutambuliwa,” kilisema chanzo.

Baadhi waliwataka Bw Joho achukue uongozi wa chama na kuwania urais au kwa njia moja au nyingine awe mshirika wa Rais Ruto katika uchaguzi ujao.

Kauli ya Waziri wa Ushirika na aliyekuwa Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya, wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo, kwamba alikuwa tayari kuondoka ODM ikiwa hilo lingesaidia kuunganisha eneo la Magharibi, ilidhihirisha mkanganyiko unaowakabili viongozi wengi waliokwama kati ya uaminifu wa chama na siasa za kikanda.

Kwa Rais Ruto, kusambaratika kwa ODM ni fursa na hatari kwa wakati mmoja. Kuwajumuisha viongozi wa upinzani katika kampeni zake kunaweza kupanua muungano wake wa kisiasa, hasa Magharibi na Nyanza.