ODM yamkemea Ruto kwa kulazimisha Wakenya kulipa ushuru wa nyumba
GEORGE ODIWUOR na JURGEN NAMBEKA
ZAIDI ya wabunge wanne wa chama cha ODM wamemtaka Rais William Ruto aheshimu uamuzi wa korti ambao uliharamisha makato ya Ushuru wa Nyumba pamoja na kupelekwa kwa polisi wa Kenya nchini Haiti.
Wabunge Lillian Gogo (Rangwe), James Nyikal (Seme), Badi Twalib (Jomvu), na Mwakilishi wa Kike, Ruth Odinga walisema kuwa huenda ikalazimu raia kurejelea maandamano iwapo Rais ataendelea na ukaidi wake wa kupuuza amri za korti kuhusu masuala hayo mawili.
Kwenye mkutano wa kusajili wanachama wa ODM katika Shule ya Upili ya Makande, Mombasa Jumapili, Januari 27, 2024 kinara wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga aliilaumu serikali ya Kenya Kwanza kwa kukata mshahara wa Wakenya kwa lazima ili kujenga nyumba za bei nafuu.
“Hata sisi katika mrengo wa Azimio tulikuwa na mpango wa nyumba za bei nafuu katika manifesto yetu. Lakini hatukunuia kukata wafanyakazi mshahara ili kuufanikisha. Wadau walifaa kuitwa ili wajadili ni namna gani mpango huo ungefanikishwa.”
Kiongozi huyo wa ODM alishutumu ukosefu wa uwazi katika mradi huo hasa kuhusu nani angenufaika nao.
“Je, ni nani anayefaa kunufaika na nyumba za bei nafuu? Hakuna sheria iliyo wazi kuhusu hilo.”
Bw Odinga pia alifokea serikali vikali kwa kuwabomolea wakazi nyumba zao katika eneo la Changamwe, Mombasa mnamo Ijumaa.
Mamia ya familia hazina makazi baada ya serikali kubomoa nyumba zao ikisema inataka kujenga nyumba za bei nafuu mahali hapo.
“Unawabomolea nyumba ilhali huna mahali mbadala pa kuwapeleka. Huo ni unyama,” akasema Bw Odinga.
Naye mbunge wa Jomvu, Bw Twalib aliipongeza mahakama kwa kusitisha makato ya nyumba.
“Ruto anafaa aheshimu uamuzi wa mahakama. Tunaipongeza mahakama kwa uamuzi huo.”
Ijumaa, Mahakama ya Rufaa iliamrisha kuwa Ushuru wa Nyumba ni haramu hivyo basi kuitaka serikali ikome kukata Makato ya Nyumba mara moja.
Ijumaa hiyo, Mahakama Kuu pia ilizima kutumwa kwa takriban maafisa 1,000 wa polisi hadi Haiti kupambana na magenge ili kurejesha amani katika taifa hilo.
Jaji Enock Chacha alisema ni wanajeshi pekee (KDF) ndio wanaweza kutumwa nje ya nchi.
Bi Gogo, hata hivyo, amemtaka Rais aheshimu korti na serikali itupilie mbali mradi huo wa ujenzi wa nyumba.
“Korti ilishatoa uamuzi kuhusu masuala hayo ambayo yanahusu umma na kusema hayazingatii sheria. Kile ambacho ni haramu hakifai kulazimishiwa raia,” akasema Bi Gogo.
Mbunge huyo alisikitika kuwa sasa ni wazi Rais anaendelea na jitihada zake za kudhibiti idara ya mahakama hasa baada ya kutoa matamshi makali kuwa ufisadi umekita kambi katika idara hiyo.
Alikashifu mazungumzo yaliyoandaliwa kati ya Dkt Ruto na Jaji Mkuu Martha Koome kuhusu madai hayo ya ufisadi.
Dkt Nyikal alimkumbusha Rais kuwa ni mahakama hiyo hiyo anayoipiga vita iliyoamua kuwa alichaguliwa kihalali baada ya kura ya Agosti 2022.
“Kama ameamua kupinga uamuzi wa mahakama, basi hata Wakenya wana haki ya kumpinga,” akasema mbunge huyo wa Seme.
Dkt Nyikal anayehudumu muhula wake wa tatu alisema kuwa ni watumishi wa umma ndio wameonyesha mfano mbaya na kuwafanya Wakenya nao pia wakaidi amri za korti.
Bi Odinga alimshutumu Rais kwa kushindwa kuteremsha gharama ya maisha huku akiendelea kuwalimbikizia Wakenya ushuru.
Bi Odinga, dada yake Bw Raila Odinga, alisema Rais Ruto hasikii tena kile anachoambiwa na Wakenya.
Baada ya korti kutoa amri kuhusu Ushuru wa Nyumba mnamo Ijumaa, Rais Ruto ambaye alikuwa ziarani katika Kaunti ya Meru alisema liwalo na liwe, pesa za Wakenya zitaendelea kukatwa.
“Ningependa kuwaambia kuwa tuko katika mchakato wa kuandaa sheria kuongoza mchakato wote unaohitajika. Pia tutakata rufaa ili mpango huo uendelee na mamilioni ya vijana wapate ajira,” akasema katika soko la Kangeta, Igembe ya Kati.