ODM yahofia mgawanyiko, yaahirisha NDC hadi mwaka ujao
HOFU ya mpasuko chamani na kuondolewa kwa Katibu Mkuu Edwin Sifuna huenda zilisababisha ODM kuahirisha Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) ambalo lilipangiwa kufanyika mwezi ujao.
Baada ya kuandaa uchaguzi wake wa mashinani, ODM ilikuwa imeratibisha kongamano hilo liandaliwe Oktoba 14 kuwachagua maafisa wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Hata hivyo, sasa kongamano hilo halitakwepo huku duru kutoka chama hicho zikiarifu kuwa, maafisa wapya watachaguliwa ndani ya robo ya kwanza ya mwaka ujao.
Jana, Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga ambaye ni Gavana wa Homa Bay alisema chama hicho sasa kitaadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake badala ya kuandaa NDC.
ODM ilianzishwa mnamo 2005 kutokana na kampeni za mrengo wa upinzani uliokuwa ukipinga rasimu ya Katiba Mpya na kupokezwa nembo ya ‘Chungwa’.
Habari kuwa kongamano hilo halitakuwa pia zilithibitishwa na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi ambao ni manaibu wa kinara wa chama hicho Raila Odinga.
“Kamati ya chama imeweka Oktoba kama mwezi ambapo kongamano la kitaifa litaandaliwa na maafisa wapya kuchaguliwa na mwelekeo mpya kutolewa,” akasema Bw Sifuna baada ya mkutano wa kamati ya ODM iliyoandaliwa mwezi uliopita.
Bw Sifuna amekuwa mwiba kwa ushirikiano wa ODM na UDA ndani ya Serikali Jumuishi na wandani wa Bw Odinga wamekuwa wakimshinikiza aondoke chamani huku wakishutumu kwa kuendeleza ajenda ya upinzani.
Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga, kakaye Bw Odinga, mara si moja katika mikutano ya hadhara, amemkashifu Bw Sifuna na kumtaka aondoke ODM huku akisema chama kinashirikiana na utawala wa Rais Ruto kwa ajili ya kupata miradi ya maendeleo kwenye ngome zake.
“Hatuwezi kuwa na katibu wa chama ambaye anafikiria yeye ndiye yumo kwenye ngazi ya juu ya utawala wa chama. Kama anajiona mbabe, basi ashauriane na Ababu Namwamba (waziri wa zamani na aliyekuwa katibu wa ODM) ili aelewe kilichomfanyikia. Sifuna anastahili kuondoka ODM,” akasema Dkt Oginga mnamo Julai 29 katika Kaunti ya Siaya.
Kwenye kundi la Dkt Oginga ni Bi Wanga, Mbunge wa Homa Bay Mjini Opondo Kaluma na Waziri wa Fedha John Mbadi miongoni mwa viongozi wengine hasa kutoka Luo Nyanza.
Wandani wa Bw Odinga ambao hawajapendezwa na Bw Sifuna, walikuwa wakilenga kutumia uchaguzi wakati wa NDC kumtimua huku duru zikiarifu nafasi hiyo ingemwendea Mbunge wa Nyando Jared Okello au mbunge mwingine asiyekuwa na msimamo mkali kutoka Magharibi mwa nchi.
Bw Sifuna tayari anaonekana amechukua mkondo wa kutaliki chama baada ya kuanzisha vuguvugu la Kenya Moja pamoja na wanasiasa wengine chipukizi akiwemo Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Gathoni Wamucomba (Githunguri), Caleb Amisi (Saboti), Anthony Kibagendi wa Kitutu Chache Kusini miongoni mwa wabunge wengine.
Duru zilieleza Taifa Leo jana kuwa, hofu ya chama kusambaratika na kusalia kigae zilichangia NDC kuahirishwa.
Baadhi walihisi kuwa iwapo Bw Sifuna atafurushwa, ODM itapata pigo magharibi mwa nchi kwa kuwa kuna hofu baadhi ya viongozi wangehama na kumfuata katika makao yake mapya.
Wengine walihisi kuwa kwa sasa chama kina ubabe mkali kati ya viongozi wake na kongamano hilo lingeingiliwa na wanasiasa kutoka nje na baadhi ya viongozi ambao wangeishia kuchaguliwa hawangekuwa waaminifu kwa chama.
Kwa hivyo, kuchelewesha uchaguzi huo kunatarajiwa kupunguza taharuki ndani ya chama ili kukipa nafasi bora ya kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa 2027.
“Hatutaki kuchanganya maadhimisho na masuala ya ndani ya chama kwa sababu tunatarajia hata waliokuwa wanachama wa zamani wajiunge nasi wakati wa sherehe hizi,” akasema Bw Osotsi.
“Tungepoteza thamani ya maadhimisho haya iwapo tungeyachanganya na NDC na uchaguzi. Tunataka wanachama wetu washerehekee, watathmini hatua ambazo chama kimepiga na kuangalia jinsi ya kukiimarisha kabla ya kura ya 2027,” akaongeza Seneta huyo wa Vihiga.
Seneta huyo aliwataka viongozi wa nyanjani na wajumbe wa chama wawe watulivu, akiahidi kuwa watapata nafasi ya kuwachagua viongozi wa kitaifa wa ODM.
Bw Nassir naye alipuuza kuwa NDC ilipanga kuwafurusha baadhi ya viongozi akisema kuwa viongozi walioteuliwa juzi wangepewa nafasi zao rasmi ili wakitumikie chama.
Mabw Osotsi, Nassir na Gavana wa Kisii Simba Arati waliteuliwa manaibu wa chama huku Bi Wanga akiteuliwa mwenyekiti.
Mabadiliko hayo yalichochewa na Opiyo Wandayi, Wycliffe Oparanya na John Mbadi kuteuliwa mawaziri katika serikali ya Rais Ruto baada ya maandamano ya Gen Z mwaka jana.