Habari za Kitaifa

Ogamba: Bodi simamizi ya Butere Girls haijavunjwa

Na RUTH MBULA April 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Elimu Julius Ogamba, Ijumaa, Aprili 11, 2025 alikanusha kuwa bodi ya Usimamizi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere imevunjwa.

Waziri Ogamba alikuwa akifafanua madai yaliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii kwamba bodi hiyo ilivunjwa kutokana na vurugu iliyoletwa na mchezo wao wa ‘Echoes of War’ katika Tamasha ya Kitaifa ya Nyimbo na Michezo ya Kuigiza Kaunti ya Nakuru.

Waziri huyo alikuwa akihutubia wanahabari katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Ichuni katika Kaunti ya Kisii wakati wa tamasha ya kuwatunuku zawadi walimu wa eneobunge la Nyaribari Masaba.

“Hayo yote ni porojo. Wakati mwingine watu huandika vitu kisha kuhusisha watu,” alisema.

Alieleza kuwa hata angevunja bodi hiyo basi hangefanya kiholela bali angefuata taratibu ili kujua nani alifanya kosa gani, vipi, wapi na kwanini.

“Huwezi tu kuamka na kupiga marufuku shirika ambalo limeanzishwa. Wako ofisini tunapozungumza na watakuwa na mkutano Jumatatu,” Waziri huyo alisema.

Wanafunzi hao walihangaishwa kuelekea siku ya kuonyesha mchezo huo huku mwandishi na mwelekezi wake seneta wa zamani Kakamega Cleopas Malala akipata agizo la mahakama lililopuuzwa na polisi.

Awali, serikali ilikuwa imepiga marufuku mchezo huo.

Jaji Mkuu Martha Koome alikuwa miongoni mwa waliolaani tukio hilo.

“Kilichotokea leo kinatutahadharisha kuhusu mwenendo ambapo amri za Mahakama Kuu zinapuuzwa. Kukataa kutii amri za mahakama hakudhuru tu mamlaka ya korti, bali pia kuna hatari kubwa kwa utawala wa sheria, ambao ni msingi wa jamii yetu,” akasema Bi Koome.

Jaji Mkuu alisema kwamba jambo linalotia wasiwasi zaidi ni taarifa za matumizi ya nguvu dhidi ya watoto wa shule.

Alhamisi, Aprili 10, 2025, saa moja na dakika ishirini asubuhi, wasichana wa Butere walifika na kupokelewa kwa shangwe na umma na wanafunzi wenzao waliokuwa wakisubiri kushuhudia tamthilia hiyo.

Tamasha za Kitaifa za Nyimbo na Michezo ya Kuigiza 2025, zilifanyika katika Ukumbi wa Melvine Jones Academy, Nakuru.

Wanafunzi walijitokeza jukwaani, wakaimba wimbo wa taifa, kisha wakaondoka kwa hasira na kutaka Bw Malala aachiliwe huru.

Waziri Ogamba pia alimlaumu mwandishi wa mchezo huo ambaye alidai kuwa alibadilisha maudhui ya awali ili kujumuisha simulizi ambalo halifai kuigizwa na watoto.

“Maudhui ya mchezo huo wa kuigiza yalibadilishwa. Walipokwenda mahakamani, mahakama iliwaruhusu kuigiza ya awali, siyo iliyobadilishwa, naomba uisome amri hiyo, kuna aya inasema waliruhusiwa kuigiza ya awali,” alisema Waziri huyo.

Mchezo huo unahusu mgogoro wa vizazi, mabadiliko ya kijamii, na athari za teknolojia, masuala ambayo ni ya kisasa na yanahusiana na hali ya kisiasa na kijamii nchini Kenya. Mchezo huo, aidha, unaangazia mapambano ya vijana dhidi ya mifumo ya utawala inayotawaliwa na hasa jinsi vijana wanavyokutana na upinzani wanapojaribu kupinga hali ya kawaida.

Mustafa, mhusika mkuu wa mchezo, anawakilisha vijana wenye ujuzi wa kiteknolojia.