Okiya akimbia kortini kupinga mkataba wa Ruto na Trump
SENETA wa Busia, Okiya Omtatah, amefika kortini kujaribu kuzuia utekelezaji wa makubaliano ya afya ya thamani ya zaidi ya Sh208 bilioni kati ya Kenya na Amerika, yaliyotiwa saini Desemba 4, 2025.
Makubaliano haya, yalisainiwa kwa niaba ya Kenya na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na kushuhudiwa na Rais William Ruto, na yanatarajiwa kutoa ufadhili wa takriban Sh208 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano kwa sekta ya afya nchini, kusaidia upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.
Hata hivyo, Seneta Omtatah anasema mchakato wa kuandaa na kusaini makubaliano haya, asili ya masharti yake, na ujumuishaji wake katika mfumo wa fedha za umma na usimamizi wa afya nchini, unakiuka vifungu vya katiba na sheria, hivyo kudhoofisha uhuru wa taifa, ushiriki wa wananchi, na haki ya kikatiba kupata huduma bora za afya.
“Mlalamishi anasikitika kwa sababu uamuzi wa kuidhinisha na kusaini makubaliano haya ulifanywa bila usimamizi wa Bunge, mashauriano ya umma, au tathmini ya wazi ya athari za kifedha,” alisema Omtatah.
Seneta huyo alisisitiza kuwa makubaliano hayo yamepangwa na kutekelezwa kinyume na kanuni za katiba zinazohusu ushiriki wa umma, uwazi, na uwajibikaji.
Hii ni kesi ya pili kufuatia ya Shirikisho la Watumiaji BidhaaKenya (Cofek) ambalo linaomba agizo la kuzuia makubaliano hayo kutekelezwa hadi kesi itakapoamuliwa.
Omtatah anasema chanzo kikubwa cha ufadhili nje ya bajeti kwa sekta ya afya nje ya mfumo wa Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma 2012 ni kinyume cha katiba.
Aidha, anataka korti itambue kuwa makubaliano haya ni mkataba wa kimataifa unaohitaji idhini ya Bunge chini ya kifungu cha 132(4) cha katiba na Sheria ya Kutayarisha na Kuidhinisha Mikataba.
Cofek pia imetaka korti izuie serikali kushiriki au kuhamisha data ya matibabu au ya kiafya kwenda Amerika au kwa mashirika yake hadi kesi itakapoamuliwa.
Shirikisho hilo linasema serikali tayari imeanza hatua za kutekeleza makubaliano hayo, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya mifumo ya kubadilishana data na mashirika yanayoweza kuhamisha taarifa za afya za raia wa Kenya hadi Amerika.
Shirikisho linasema utekelezaji wa makubaliano haya umefanywa bila kufuata Sheria ya Ulinzi wa Data, Sheria ya Afya ya Kidijitali, Sheria ya Afya, na Kanuni za Kubadilishana Data za Afya za Kidijitali (2025), ambazo zinahitaji ulinzi mkali kabla ya kuhamishwa kwa data yoyote ya afya kwenda nje ya nchi.
Omtatah na Cofek wanasema makubaliano hayo yanahitaji Kenya kutoa data kubwa za matibabu na kiafya, ikiwemo taarifa za Ukimwi, kifua kikuu, malaria, afya ya akina mama, na ufuatiliaji wa magonjwa, ambayo ni maelezo nyeti ya mamilioni ya wananch na sehemu ya miundombinu ya usalama wa afya ya taifa.
Shirikisho linasema makubaliano haya hayajakidhi kanuni za utawala bora chini ya kifungu cha 10 cha katiba, jambo linalokiuka thamani za uwajibikaji, uwazi, ushiriki wa wananchi, na uadilifu.
Aidha, kuhamishwa kwa data hizi kunatishia kuvunwa kwa faragha, ubaguzi, na matumizi mabaya ya taarifa.
Cofek imesema hatua za korti zinahitajika haraka ili kuzuia madhara yasiyoweza kurekebishwa, na kwamba utekelezaji wa makubaliano haya bila ushauri wa Bunge unakiuka katiba na unaleta hatari kubwa kwa wananchi na taifa.