• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:25 PM
Ombi la kutimua Jaji Esther Maina lawasilishwa JSC

Ombi la kutimua Jaji Esther Maina lawasilishwa JSC

Na RICHARD MUNGUTI

OMBI la kumtimua Jaji Esther Maina anayesimamia kitengo cha Mahakama Kuu cha kuamua kesi za ufisadi limewasilishwa siku moja baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagu kumnyooshea kidole cha lawama kufuatia agizo alilotoa 2020 la kutwaliwa kwa Sh202 milioni aliposhtakiwa kwa ufisadi wa Sh7.3 bilioni.

Hivi punde kumekuwa na malumbano makali kati ya serikali kuu na idara ya mahakama huku Rais William Ruto akidai kuna majaji wafisadi wanaopokea rushwa kutoka kwa wapinzani wa Serikali ya Kenya Kwanza kutoa maagizo ya kusambaratisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na chama tawala za Kenya Kwanza kulingana na manifesto yake.

Katika kesi iliyowasilishwa na Bw Antony Kefa Odiero kwa tume ya kuajiri watumishi katika idara ya Mahakama-JSC, Jaji Maina amedaiwa aliitisha hongo alegeze makali ya agizo la kutwaliwa kwa pesa zake Sh53 milioni na magari yake mawili ya kifahari yenye thamani ya mamilioni ya pesa.

Kupitia kwa kampuni ya mawakili ya Ndegwa & Ndegwa Advocates, Bw Odiero anadai Jaji Maina alimwitisha hongo ya Sh2.5milioni kupitia kwa Mbunge wa zamani Bw Antony Manyara.

Bw Odiero aliyewasilisha kesi hiyo chini ya kifungu cha Katiba Nambari 172 anaomba JSC ichunguze tabia ya Jaji huyo na kumtimua kazini ili kuhifadhi heshima na jina nzuri la Idara ya Mahakama.

Mlalamishi huyo anadai kuwa mnamo Agosti 25, 2023 mamlaka ya serikali ya kutwaa mali zilizonunuliwa kwa pesa za umma zilizoibwa (ARA) ilipata agizo la kutwaa Sh53 milioni na magari mawili ya Bw Odiero. Agizo hilo lilitolewa na Jaji Diana Kavedza aliyeamuru kesi hiyo isikizwe na Jaji Maina.

“Mnamo Septemba 6, 2023 nilipokea simu kutoka kwa Bw Antony Manyara kuhusu kesi niliyoshtakiwa na ARA. Alitaka tukutane katika Jaffery Sports Ground saa mbili na nusu usiku kunipa ujumbe wa Jaji Maina,” Bw Odiero amedai katika ushahidi aliowasilisha kwa JSC.

Mlalamishi huyo amedokeza kuwa walikutana kisha akafahamishwa ujumbe wa Jaji Maina kwamba ampe Bw Antony Manyara Sh2.5 milioni ampelekee ndipo alegeze maagizo ya kutwaa pesa hizo na magari yake.

Kwa mujibu wa Bw Odiero, Bw Manyara alidai ndiye anatumwa na Jaji Maina kumchukulia hongo.

Bw Odiero amedai alifahamishwa awasilishe ombi akitaka aruhusiwe kuchukua pesa pesa za kulipia watoto karo ya shule na mahitaji mengineyo.

Mlalamishi amedai alielezwa akikosa kutoa pesa hizo atajilaumu mwenyewe.

Bw Odiero anasema alikataa kutoboka hongo hiyo na alipowasilisha ombi lilitupiliwa mbali na Jaji Maina mnamo Septemba 8, 2023.

Hivi majuzi Bw Gachagua alinukuliwa na vyombo vya habari akisema Alhamisi Januari 18, 2024 hii atawasilisha kesi dhidi ya Jaji Maina kutokana na agizo la kutwaa pesa zake Sh202 milioni mnamo Juni 2020.

Jaji Maina aliamuru Sh202 milioni za Bw Gachagua zitwaliwe alipokuwa Mbunge wa Mathira kabla ya kuteuliwa na Rais William Ruto kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Ombi la kutwaliwa kwa pesa hizo za Bw Gachagua liliwasilishwa na mamlaka ya serikali ya kutwaa mali zilizonunuliwa na pesa zilizoibwa kutoka kwa Serikali (ARA).

ARA ilieleza Jaji Maina kwamba akaunti tatu za benki za Bw Gachagua zilikuwa na Sh7.3 bilioni na zilitumika kukopa Sh12.5bn kati ya miaka ya 2013 na 2020.

Pesa hizo Jaji Maina alifahamishwa na ARA zilidhaniwa zilipatikana kwa njia ya ufisadi.

Mahakama ilielezwa Juni 2020 kwamba Bw Gachagua na mfanyabiashara mwenzake Bi Anne Kimemia katika kampuni ya Jenne Enterprises Ltd walishindwa kueleza jinsi walijipatia Sh202 milioni zilizokuwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo.

Akaunti nyingine ya Bw Gachagua katika benki ya Rafiki Micro Finance Bank ilikuwa na Sh165 milioni.

Pia katika akaunti iliyokuwa katika Benki ya Rafiki Micro Finance ilikuwa na Sh35 milion na akaunti ya tatu
ilikuwa na Sh773,228.

Akaunti ya kampuni yao Jenne Enterprises ilikuwa na Sh1.1 milioni.

JSC itatoa mwelekeo kuhusu ombi hilo dhidi ya Jaji Maina.

  • Tags

You can share this post!

Ruto akataa ‘kukaliwa chapati’

Mauaji: Kawira asisitiza ukweli utabainika, uongo uyoyomee...

T L