Omtatah ashikana na maseneta 21 kurudi kortini kujaribu kuangusha tena Ushuru wa Nyumba
Na RICHARD MUNGUTI
SENETA Okiya Omutatah na maseneta wengine 21 wamerudi tena mahakama kukabana koo na Rais William kuhusu sheria ya kodi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu wanayodai ni haramu na kwamba inakinzana na Katiba.
Maseneta hao Okiya Omutatah, Stewart Madzayo, Enock Wambua, Ledama ole Kina, Edward Sifuna, Okong’o Omogen, Kajwang Moses Otieno, Godfrey Osotsi, Mohamed Faki Mwinyi Haji, Johnes Mwaruma, Crystal Asige, Dan Maanzo, Agnes Kavindu Muthama, Oburu Odinga, Richard Onyonka, Beatrice A Oyomo, Catherine Muyeka Mumma, Hamida Kibwana, Hezena Lamaletian, Dr Beth Kalunda Syengo, Shakila Abdalla Mohamed na Eddy Gicheru Oketch wanaomba mahakama kuu itumie uwezo na mamlaka iliyopewa na Kifungu Nambari 165 cha Katiba kuwakomboa Wakenya na kile walichosema ni “utumwa mambo leo”.
Katika kesi hiyo iliyoratibishwa kuwa ya dharura na Jaji Enock Chacha Mwita, maseneta hao wanaomba jopo la majaji wasiopungua watano wateuliwe kutathmini mchakato mzima wa sheria ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu wanayosema ilipitishwa kwa pupa kabla ya kupigwa msasa na Bunge la Seneti.
Ombi kuu ni kuharamishwa kwa sheria hiyo ya kodi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu iliyopitishwa na bunge na kutiwa sahihi na Rais William Ruto Machi 24, 2024.
Maseneta hao wamesema kodi hii inawakandamiza Wakenya na suluhu ni mahakama kuu kuiharamisha.
Kuiratibisha ya dharura
Baada ya kuiratibisha kuwa ya dharura, Jaji Mwita aliwaamuru Bw Omtatah na wenzake wawakabidhi washtakiwa wanaojumuisha Mwanasheria Mkuu, Mabunge ya Seneti na Bunge la Kitaifa, Mawaziri wa Ardhi na Nyumba, Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA), Baraza la Magavana (CoG), Kamishna wa Forodha na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) na nakala za kesi hii ili wajibu madai ya ukiukaji wa sheria na utozaji Wakenya ushuru wa kugharamia ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
Jaji Mwita aliamuru kesi hiyo itajwe mbele yake Aprili 11, 2024 kwa maagizo zaidi kutolewa.
“Kesi hii inazua masuala mazito ya kisheria na yapasa kusikizwa upesi na masuala tata ya sheria kusuluhishwa,” Jaji Mwita alisema huku akiratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura.
Katika kesi hiyo, maseneta wamesema kwamba sheria ya kuwatoza wananchi kodi ya nyumba za bei nafuu iliharakishwa kutiwa sahihi na Rais Ruto kabla ya kuidhinishwa na Bunge la Seneti.
Maseneta hao wamekosoa sheria hiyo wakisema imempa mamlaka Kamishna wa Masuala ya Kodi kutoza Wakenya kodi ilhali hana mamlaka kisheria kupokea kodi kutoka kwa wananchi.
Pia wamelalamika kwamba Rais Ruto alitumia sheria hii ya kodi ya nyumba kubadilisha Katiba kuhusu sheria ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
Ardhi ya umma ‘kunyakuliwa’
Wanasiasa hawa wamesema kupitishwa kwa sheria hii mpya ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu umehalalisha utumizi wa sheria nambari 84 ya Sheria za Fedha 2024 iliyokuwa imeharamishwa na majaji watatu wa mahakama kuu.
Maseneta hawa wameomba kesi hii iwasilishwe mbele ya Jaji Mkuu kuwateua majaji zaidi ya watatu watakaosikiza kesi hii.
Mahakama inaombwa iharamishe sheria hii kwa vile ‘imekubalia’ ardhi ya umma ‘kunyakuliwa’ na kujengwa nyumba ambazo hatimaye zitauziwa watu binafsi.
Wanasiasa hawa pamoja na wanaharakati watano wamesema serikali ya Rais Ruto imekaidi katiba kwa kupitisha sheria ya kuwatoza wananchi kimakosa na mahakama kuu inapasa kupiga breki utekelezaji wa sheria hii kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii.
Maseneta hao wamezua masuala zaidi ya 30 wanayosema Mahakama kuu ikiyajibu barabara bila shaka sheria hiyo itaharamishwa.
Wanasiasa hao pamoja na wanaharakati Eliud Karanja Matindi, Benson Odiwuor Otieno, Blair Angima Oigoro, Victor Okuna, Florence Kanyua Lichoro, Juma John Isaac na Mbunge wa zamani Alfred Keter wamesema hakuna bodi ya kudhibiti ukusanyaji na matumizi ya pesa hizo.
Pia wanasema Rais Ruto aliamuru ardhi ya umma itwaliwe kujenga nyumba hizo ambazo mwishowe zitauziwa watu binafsi.
“Wananchi watapoteza ardhi yao kutokana na ujenzi huu wa nyumba. Hatimaye hakutakuwa na ardhi ya umma,” wanalalamika maseneta na wanaharakati katika ushahidi waliowasilisha mahakamani.
Jaji Mwita atatoa mwelekeo Alhamisi kuhusu kesi itakayotimbua kivumbi na kujua mbivu na mbichi katika serikali ya Kenya Kwanza.