Ongezeko la matukio ya vita kati ya polisi na KDF lazua hofu
NA VALENTINE OBARA
WANANCHI wameeleza wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya makabiliano kati ya maafisa wa polisi na wanajeshi nchini.
Katika kisa cha majuzi zaidi, makabiliano yalizuka kati ya maafisa wa polisi na wanajeshi wa KDF katika kivuko cha feri Likoni, Kaunti ya Mombasa.
Video iliyosambazwa mitandaoni ilionyesha kundi la wanajeshi wakipigana na maafisa wa polisi wanaodumisha ulinzi na usalama katika feri, pande zote mbili zikiwa na silaha.
Mmoja wa wanajeshi alionekana pia akimzaba kofi afisa wa kampuni ya kibinafsi ya ulinzi, huku baadhi ya polisi na wanajeshi wakijaribu kuingilia kati na kutuliza hali.
Haikubainika mara moja chanzo cha kisa hicho ingawa gari la jeshi lilionekana limesimama hapo ikiaminika lilikuwa likisubiri kuvuka hadi upande wa pili.
Kupitia kwa taarifa, Jeshi la Ulinzi wa Taifa (KDF) lilithibitisha kisa hicho cha Jumamosi jioni na kusema uchunguzi utafanywa kubaini chanzo chake.
“Kisa hicho ni cha kusikitisha. Kama maafisa wa KDF, tunafaa kufuata kikamilifu maadili yetu ya utendakazi,” taarifa hiyo ikasema.
Kisa hicho ni cha tatu cha aina yake kutokea ndani ya wiki mbili. Mnamo Aprili 17, makabiliano yalitokea kati ya polisi na wanajeshi Lodwar, Kaunti ya Turkana.
Wanajeshi karibu 10 walivamia kituo cha polisi kuokoa wenzao waliokuwa wamekamatwa walipomshambulia afisa wa polisi barabarani na kumpokonya bunduki yake.
Hata hivyo, KDF ilikana ripoti hizo lakini ikaongeza kuwa uchunguzi utafanywa. Katika Kaunti ya Kilifi, afisa wa jeshi aliwekwa kizuizini alipomshambulia afisa wa polisi kituoni.
Kulingana na ripoti ya polisi, afisa huyo wa jeshi alikuwa ameenda katika kituo cha polisi kumtoa jamaa yake seli kwa lazima.
Ripoti hiyo ilisema mwanajeshi huyo akiandamana na mjomba wake, walivamia kituo kidogo cha polisi cha Bindira ili kumwondoa seli mshukiwa aliyekuwa amekamatwa kwa kosa la kumpiga mtu.
Kando na kumpiga na kumjeruhi afisa wa polisi aliyekuwa kituoni, wawili hao walilaumiwa pia kwa kuvunja mlango na dirisha la kituo hicho cha polisi ili kumwezesha mshukiwa kutoroka.
“Walimgeukia pia mlalamishi ambaye alikuwa kituoni, wakamkwida katika jaribio la kumnyonga na kumpiga katika afisi ya kuandikisha ripoti,” taarifa hiyo ikaeleza.