Habari za Kitaifa

Onyo la Serikali kwa Wakenya wanaoishi Tanzania

Na BENSON MATHEKA December 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Wakenya wanaoishi Tanzania wameonywa kuwa waangalifu na makini zaidi  kufuatia ripoti za uwezekano wa ghasia wakati wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Uhuru wa nchi hiyo mnamo Desemba 9, 2025.

Serikali ya Tanzania imefuta sherehe hizo kufuatia hofu ya kuzuka kwa maandamano.

Kwenye taarifa iliyotolewa Ijumaa, Desemba 5, 2025, Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania uliwahimiza Wakenya wanaoishi katika nchi hiyo jirani kuchukua tahadhari kuhakikisha usalama wao.

Wakenya walioko nchini humo waliambiwa wabaki ndani ya nyumba iwapo kutakuwa na taarifa za ghasia na kuepuka usafiri usio wa lazima isipokuwa iwe ni muhimu.

Walionywa pia kuepuka mikusanyiko mikubwa, maandamano, na vituo vya usalama. “Hali inaweza kubadilika haraka,” ubalozi ulionya.

“Fuatilia njia rasmi za habari na mitandao/ tovuti ya ubalozi kwa taarifa sahihi na za wakati halisi. Usitegemee uvumi usiothibitishwa,” sehemu ya taarifa hiyo ilisema.

Ubalozi pia uliwahimiza Wakenya wanaoishi Tanzania kuwa na mpango wa mawasiliano tayari na familia na marafiki kutokana na ripoti za uwezekano wa kuzimwa kwa huduma za intaneti na simu za mkononi.

Zaidi ya hayo, Wakenya walio nchini humo walitakiwa kuhakikisha wana chakula cha kutosha, maji, dawa muhimu, na simu ya mkononi yenye chaji.

“Iwapo unahitaji msaada au huduma za kidiplomasia, wasiliana na namba zetu za dharura: [+255-690-283-011 au +255-690-283-012] na barua pepe: [email protected],” ubalozi uliwashauri.

Ubalozi pia uliwahimiza watu kuhakikisha kuwa stakabadhi zao za usafiri au makazi ziko sahihi na zinazingatia sheria na kanuni za Tanzania.

Taarifa hii ya dharura kutoka serikali ya Kenya ilitolewa kufuatia ripoti za maandamano yanayopangwa dhidi ya serikali nchini Tanzania mnamo Desemba 9, kwa lengo la kulaani mauaji yaliyotokea baada ya uchaguzi mwishoni mwa Oktoba na mapema Novemba mwaka huu.

Hata hivyo, polisi wa Tanzania wamepiga marufuku maandamano hayo na kuonya yeyote atakayesababisha  ghasia katika sehemu yoyote ya nchi.