Habari za Kitaifa

Operesheni kali aliyoahidi Murkomen yanasa wezi 12 wa mifugo Mlima Kenya

Na MWANGI MUIRURI September 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WASHUKIWA 12 wa wizi wa mifugo katika maeneo kadhaa ya Kati mwa Kenya wamekamatwa ndani ya muda wa saa 24 zilizopita kufuatia operesheni iliyoendeshwa na walinda usalama.

Hatua hiyo ilichukuliwa mwezi mmoja baada ya wakulima kulalamikia wizi wa mifugo na mazao yao.

Kulingana na mkakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo uliotolewa na Kamati ya Usalama Ukanda wa Kati ikiongozwa na Joshua Nkanatha, maafisa wa usalama wanalenga makundi saba wa wahalifu wanaohusishwa na wizi huo.

Inaripotiwa kuwa makundi hayo yanajumuisha manaotoa habari za kijasusi—hasa majirani ya wakulima na wafugaji—hadi wale wanaotekeleza uvamizi.

“Majasusi wanashirikiana na mabroka wanaoshirikisha safu ya tatu inayoshirikisha wahalifu kamili wanaotekeleza uvamizi,” ripoti hiyo inaeleza.

Baada ya mifugo kuibiwa, wasafirishaji kwa kutumia magari na pikipiki hupeleka mali hiyo haramu masokoni.

“Kupatikana kwa masoko hufanikishwa na baadhi ya maafisa wa usalama, ambao katika vizuizi au vituo vyao, hukusanya hongo kuruhusu uhalifu huo kuendelea,” ripoti hiyo inaongeza.

Safu ya mwisho inahusisha wenye bucha na vituo haramu vya ununuzi, baadhi yakiwa ndani ya masoko rasmi.

Hata hivyo, mawakili na washukiwa wanasema kuwa operesheni hiyo haiongozwi na nia halisi ya kuzima wizi huo bali ni kifumba macho tu.

Malalamishi yameibuliwa kuhusu mwenendo wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuchapisha picha na maelezo kuhusu watu wanaodaiwa kuwa washukiwa wa wizi huo hata kabla ya wao kuwasilisha kortini kujibu mashtaka.

DCI inasema kuwa washukiwa 12 wanaozuiliwa walikamatwa kufuatia uchunguzi uliondeshwa baada ya maafisa kupokea habari za kijasusi.

Kulingana na taarifa ya DCI, washukiwa walikamatwa baada ya uchunguzi kamili kufanya “na tuliweza kuendesha operesheni katika miji ya Kagio na Mwea katika Kaunti ya Kirinyaga.”

“Watu hao wanashukiwa kuhusika na msururu wa wizi wa mifugo ambao umekithiri katika kaunti za Kirinyaga, Embu, Nyeri na Murang’a. Inaaminika kuwa wezi hao pia huwatia woga wakulima katika maeneo husika,” ikaleza taarifa hiyo.

Uchunguzi umebaini kuwa genge hilo linashirikisha wezi, wanunuzi, wasafirisha na wenye maduka ya kuuza nyama.

Kati ya waliokamatwa wanne wanaaminika kuwa sugu na wamekuwa wakiendesha uhalifu huo nje ya maeneo ya Kati na Mashariki mwa Kenya.

“Wezi hao wamewasababishia hasara kubwa wakulima na hivyo kuwafukarisha kabisa,” DCI ikaeleza.

Maafisa wa upelelezi walipata gari aina ya Probox inayotumiwa kusafirisha nyama.

Mhudumu wa bucha mjini Embu pia alikamatywa kwa kununua kilo 119 ya nyama kutoka kwa washukiwa wa wizi.