Orengo arejea kwa kishindo, atangaza yuko kidete na hang’atuki
Gavana wa Siaya, James Orengo, alitokeza hadharani kwa mara ya kwanza Ijumaa baada ya ukimya wa wiki kadhaa uliozua uvumi mwingi kuhusu mahali alikokuwa. Alihudhuria mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Karachuonyo, Bi Phoebe Asiyo, katika Kijiji cha Wikondiek, Kaunti ya Homa Bay.
Orengo alifika kwenye hafla hiyo ya mazishi saa saba unusu mchana, saa tatu baada ya Rais William Ruto na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga kuwasili. Alitua kwa helikopta katika eneo hilo la Karachuonyo wakati mwenyeji wake, Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, alipokuwa akitoa heshima zake za mwisho kwa marehemu Asiyo.
Kufika kwake kulisababisha shangwe kutoka kwa waombolezaji, huku baadhi wakimkimbilia kabla ya kuzuiwa na walinzi waliokuwa macho zaidi kutokana na uwepo wa Rais.
Kwa muda mrefu kumekuwa na tetesi kwamba Gavana Orengo alikuwa India au Amerika kwa matibabu, lakini hotuba yake kali na ya kujiamini iliwatuliza wafuasi wake na umma kwa ujumla. Ingawa hakufichua alikokuwa, aliwahakikishia wote kwamba yuko salama kiafya.
Akizungumza kwa lugha ya Dholuo, alikanusha uvumi kuwa amejiondoa mamlakani:
“An Orengo Nyatieng Angima, an Orengo Kidi onge kama adhiye, koro eka aroch marach.”
(Ikifasiriwa: “Mimi Orengo, mwamba wa Nyatieng, niko salama. Mimi ni Orengo mwamba, siendi kokote. Kwa kweli, nimejivua ngozi ya zamani na najihisi mpya kuliko awali.”)
Kisha aliendelea kutoa heshima zake kwa marehemu Asiyo:
“Mwanamke huyu, tukichunguza historia ya harakati za haki za binadamu na wanawake, Phoebe Asiyo alikuwa mbele ya wakati wetu. Alianza mapambano hayo hata kabla ya uhuru na akaendelea baadaye.”
Orengo alisema alifanya kazi naye bungeni katika kipindi ambacho wanawake walikuwa na wakati mgumu kuingia katika uongozi wa kisiasa.
“Homa Bay inaongoza kwa kuwa na wanawake wengi waliochaguliwa. Huu ni ushahidi wa mafanikio ya Asiyo.”
Alisema Bi Asiyo alikuwa mtetezi wa masuala mazito bungeni, licha ya kuwepo kwa wabunge wa kiume waliokuwa na fikra duni kuhusu uongozi wa wanawake.
“Wakati huo kulikuwa na wanaume waliojawa na chuki dhidi ya wanawake, lakini Phoebe hakuwahi kuyumba,” alisema.
Orengo pia alikosoa utamaduni wa Wakenya wa kutowatambua mashujaa wa kitaifa, akitaja kutopewa heshima kwa hayati Jaramogi Oginga Odinga kama mfano.
“Hakuna hata mnara uliotengwa kumuenzi Jaramogi, licha ya mchango wake mkubwa kwa taifa. Hili ni jambo ambalo tunafaa kulirekebisha.”
Kurejea kwa Orengo hadharani kunakomesha uvumi uliokuwa umeenea kuhusu afya na hatima yake kisiasa. Kuibuka kwake kunajiri siku tatu tu baada ya Naibu wake, William Oduol, kutoa taarifa kuhusu hali ya uongozi katika Kaunti ya Siaya, akidai kuwa hajui alipo Gavana wake.