Orengo, Nyong’o wakosa mazishi ya Were tofauti zao na Raila zikipanuka
MAGAVANA James Orengo (Siaya) na Anyang’ Nyong’o (Kisumu) jana walikosa kuhudhuria mazishi ya marehemu mbunge wa Kasipul, Charles Were hatua ambayo imezua tetesi kuhusu uhusiano wao na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ambaye alihudhuria.
Kutohudhuria kwao kumekuja wakati ambapo kuna uvumi wa kuwepo kwa mgawanyiko kati yao na Raila, hasa kutokana na matukio ya hivi majuzi ya kisiasa. Orengo na Nyong’o kwa nyakati tofauti wamekosoa waziwazi uamuzi wa Raila wa kushirikiana na Rais William Ruto.
Orengo, kwa upande wake, ameonyesha wasiwasi kuhusu ushirikiano huo mpya wa kisiasa, akidai kuwa umedhoofisha uwezo wa upinzani kuikosoa serikali ya Ruto.
Licha ya kuwa mshirika mwaminifu wa Raila kwa miongo kadhaa, Orengo amekuwa mkosoaji mkali wa makubaliano kati ya Ruto na Raila.
“Tulipigania Katiba ya kidemokrasia ambapo watu wanapaswa kusema ukweli. Nawaomba Wakenya kuwaambia viongozi wao ukweli. Nchi hii itaporomoka tena ikiwa lugha tunayosikia itaendelea,” alisema Orengo katika hafla ya mazishi ya mlinzi wa Raila Bw Oduor katika Kaunti ya Siaya.
Gavana Nyong’o alimshambulia Ruto kwa madai ya kudhoofisha ugatuzi.Katika barua kali iliyotolewa Jumanne, Aprili 22, Gavana Nyong’o, aliibua upya mvutano kati ya serikali ya kaunti na serikali kuu kuhusu usimamizi wa Hazina ya Ukarabati wa Barabara (RMLF), ambayo Rais William Ruto anasisitiza isimamiwe na serikali ya kitaifa.
Nyong’o alimshutumu Rais kwa kujaribu kutwaa mamlaka kwa nguvu, akifananisha hatua hiyo na mienendo ya kiimla enzi za siasa za zamani za Kenya.Ingawa Raila Odinga alimuunga Nyong’o kuhusu suala la RMLF, kiongozi huyo wa ODM alitofautiana na gavana huyo kuhusu mpango wa serikali wa kukodisha viwanda vya sukari kwa wawekezaji wa kibinafsi.
Serikali ya Kenya Kwanza inapanga kukodisha viwanda vinne vya sukari vinavyomilikiwa na serikali — Nzoia, Chemelil, Muhoroni na Sony Sugar – kwa lengo la kufufua sekta hiyo inayoyumba na kuinua maisha ya wakulima na wafanyakazi.Hata hivyo, pendekezo hilo limezua mjadala mkali, hasa katika eneo la Magharibi mwa Kenya.
Jumatano, Mei 9, Gavana Nyong’o alielezea mpango huo kama “mapinduzi ya kiuchumi” dhidi ya wakulima na jamii za wenyeji, akikosoa ukosefu wa ushirikishaji wa wadau muhimu.Raila, kwa upande wake, ameunga mkono mpango huo wa ukodishaji.
Katika mkutano wa hivi majuzi na Waziri wa Kilimo, Mutahi Kagwe, Raila alisifu juhudi za serikali za kufufua sekta ya sukari kupitia ushirikiano wa kimkakati.
“Raila alionyesha nia na kuunga mkono mageuzi haya, akitambua uwezo wake wa kuchochea ukuaji wa uchumi wa vijijini na usalama wa chakula,” ilisema taarifa.