Papa Francis aomboleza wanafunzi waliofariki katika mkasa wa moto Nyeri
KIONGOZI wa Kanisa la Katoliki Ulimwenguni Papa Francis ametuma risala za rambirambi kwa familia za wanafunzi 17 waliokufa katika mkasa wa moto uliotokea katika Shule ya Hillside Endarasha Academy, Kieni, Nyeri, Alhamisi usiku.
Kwenye taarifa iliyowasilishwa Jumamosi, Septemba 7, 2024 na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Jimbo la Nyeri Antony Muheria, Papa alielezea mkasa huo kama “janga” lililoathiri pakubwa taifa la Kenya.
“Ninahuzunishwa zaidi na kile kilichosababisha vifo vya watoto hawa wa umri mdogo. Mwenyezi Mungu alinde nyoyo zao na familia zao zipate nguvu za kustahimili machungu hayo,” akasema Papa Francis.
Taarifa hiyo ilitiwa saini na Katibu wa Vatican Kadinali Pietro Parolin.
Kulingana na Wizara ya Elimu bweni ambalo lilishika moto na kusababisha maafa lilisheheni jumla ya wanafunzi 152, wavulana.
Kando na watoto 21 waliokufa, zaidi ya 20 walipata majeraha mabaya ya moto na wanapokea matibabu katika hospitali mbalimbali katika kaunti ya Nyeri.
Kufuatia mkasa huo, Rais William Ruto Ijumaa alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya wanafunzi hao.
“Kama ishara ya alama iliyoachwa na nyonyo za wanafunzi hao 17 (sasa ni 21) waliokufa, nimetangaza siku tatu ya maombolezo ya kitaifa nchini Kenya,” Dkt Ruto akasema kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari.
Kiongozi wa taifa aliamuru bendera zote za Kenya na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupeperushwa nusu mlingoti ndani ya siku hizo tatu za maombolezo.
Bendera hizo zitapeperushwa katika hali hiyo kuanza Septemba 9, 2024 hadi Jumatano Septemba 11, 2024 katika Ikulu, vituo vyote vya serikali na jeshi nchini Kenya sawa na katika balozi zote za Kenya ughaibuni.