• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Passaris awapuuza waliomzomea wakati wa maandamano kukemea mauaji ya wanawake

Passaris awapuuza waliomzomea wakati wa maandamano kukemea mauaji ya wanawake

NA WANDERI KAMAU

MWAKILISHI wa Kike katika Kaunti ya Nairobi, Esther Passaris, Jumapili, Januari 28, 2024 alipuuza kundi la watu ambao walimzomea Jumamosi wakati wa maandamano ya kupinga ongezeko la mauaji ya wanawake nchini.

Bi Passaris alijipata motoni, baada ya kuzomewa na kundi la umati uliokuwa umekusanyika jijini Nairobi kuandamana dhidi ya mauaji hayo.

Baadhi ya watu walihisi kuwa licha ya kujitokeza kuungana na waandamanaji hao, hajachukua hatua za kutosha kuonyesha kujitolea kwake kukabiliana na visa hivyo kama kiongozi.

“Nadhani kuwa watu walihisi ulijitokeza ukiwa umechelewa sana kukashifu visa hivyo. Pengine huu ndio wakati mwafaka wa kuweka mikakati ya kisheria kukabiliana na kuenea kwa visa hivyo,” akasema mtu mmoja kwenye mtandao wa ‘X’.

Hata hivyo, Bi Passaris alisema kuwa watu hao walimlaumu kwani hawakuwa na mtu mwingine wa kuelekezea lawama zao.

“Si kwa sababu “sikuchukua juhudi zozote”. Nimekuwa nikishirikiana na Mashirika ya Kutetea Haki za Umma kuandaa maandamano haya tangu mipango hiyo ilipoanza,” akasema.

Akaongeza: “Mimi binafsi na washirika wangu wote tumetoa mchango wetu. Tulishiriki kwenye maandamano hayo na tukayamaliza kwa nguvu. Sasa tumerejea kazini, tukijua kuwa sote ni sehemu ya suluhisho la kudumu kuhusu tatizo hili.”

Mnamo Jumamosi, Januari 27, 2024 kundi la wanawake lilimzomea vikali Bi Passaris kwa kumwambia: “Rudi nyumbani! Ulikuwa wapi?” katika Bustani ya Jevanjee.

Kundi hilo halikumruhusu kiongozi huyo kutoa kauli yoyote, alipoalikwa kuwahutubia waandamanaji.

Baadaye, kwenye kikao na wanahabari, Bi Passaris alisema kuwa kila mmoja anafaa kushiriki kwenye juhudi za kukabiliana na mauaji hayo, wala si jukumu la viongozi wa kisiasa pekee.

 

  • Tags

You can share this post!

Ukosefu wa maji salama tishio kwa lishe na usafi –...

Dereva Jim Heather-Hayes atawazwa mwanamichezo bora mbio za...

T L