Pauni moja ya Uingereza sasa ni Sh200 katika tukio la kihistoria
Na PATRICK ALUSHULA, Business Daily
Ubadilishanaji wa sarafu za kigeni umeingia katika tukio la kihistoria Jumatano, Januari 10, 2024 baada ya pauni moja ya Uingereza kununuliwa kwa zaidi ya Sh200.
Kulingana na data ya ubadilishanaji fedha za kigeni ya Benki Kuu ya Kenya, pauni moja ya Uingereza inauzwa kwa wastani wa Sh202.46, hatua ambayo itaimarisha pakubwa pato la wauzaji bidhaa nchini Uingereza na sehemu zingine barani Uropa kwa kutumia sarafu hiyo.
Kubadilishana pauni moja kwa Sh202.46 kunamaanisha kwamba shilingi ya Kenya imepoteza thamani kwa asilimia 33.1 katika kipindi cha mwaka mmoja pekee uliopita, kwa sababu Januari 2023 ilikuwa wastani wa 150.09.
Benki kadhaa nchini, hata hivyo, zimekuwa zikiuza pauni hiyo hadi Sh218 kwa wiki nyingi, lakini sasa taarifa za Benki Kuu zinathibitisha kwamba kweli pauni moja ni zaidi ya shilingi mia mbili za Kenya.
Kenya huuza mazao ya kilimo kama maua, matunda, mboga, kahawa, chai nchini Uingereza lakini nayo hununua bidhaa kama magari, mitambo ya viwanda, pombe, dawa, vyombo vya elektroniki kutoka mataifa ya Ulaya.
Pauni kuwa ghali inamaanisha kwamba Wakenya watanufaika zaidi kwa sababu ya kiasi kikubwa cha bidhaa zinazouzwa katika mataifa ya Ulaya ikilinganishwa na bidhaa Wakenya wanazonunua katika nchi hizo.
Kudorora kwa thamani ya shilingi hivyo basi kunamaanisha kwamba wanaouza bidhaa zao nchini Ulaya watafaidi pale wanapokuja na pauni hizo kisha wazibadilishe kuwa shilingi za Kenya.
Hata hivyo, kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya ni janga kwa taifa haswa kwa upande wa kulipa mikopo kwa sababu inamaanisha kwamba deni hilo litaongezeka kuliko awali.
- Imetafsiriwa na FATUMA BARIKI