Habari za Kitaifa

Pendekezo bungeni wahasibu wa shule za umma wakaguliwe mitindo ya maisha na kuhamishwa

Na  SAMWEL OWINO August 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Wahasibu na maafisa wa fedha katika shule za umma watakaguliwa mtindo wa maisha na hata kuhamishwa baada ya kila miaka minne, iwapo Bunge la Taifa litaidhinisha mswada mpya wa marekebisho ya sheria unaoendelea kuzingatiwa.

Mswada wa Marekebisho ya Elimu ya Msingi, 2025, unapendekeza kubadilisha Sheria ya Elimu ya Msingi, Sura ya 211, ili kukuza uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya fedha za shule kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi wa Umma.

Mswada huo, uliodhaminiwa na Mbunge wa Sirisia, John Waluke, unapendekeza kuwa taasisi zote za elimu ya msingi ziwasilishe maelezo ya mapato, mali na madeni ya wafanyakazi wasio walimu, wake au waume zao, na watoto wao wanaowategemea.

“Kwa muda mrefu katika taasisi za elimu ya msingi, wahasibu ambao huajiriwa na bodi za usimamizi wamekuwa wakitumia fedha za shule kwa manufaa yao binafsi, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Maafisa wa Umma,” Bw Waluke alieleza Kamati ya Elimu ya Bunge.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, ukaguzi huu unalingana na masharti ya Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Sura ya 412B, na utaimarisha uwajibikaji katika taasisi za elimu ya msingi.

“Hii itahakikisha matumizi bora ya fedha za umma na kutekeleza haki ya kupata elimu kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 53 (1)(b) ya Katiba ya Kenya,” akaongeza.

Bw Waluke alisema kuwa kwa kuwa ni Bunge linaloidhinisha mishahara ya wahasibu hao, basi wanahesabiwa kuwa maafisa wa umma na hivyo wanapaswa kukaguliwa kikamilifu.

“Mtu yeyote anayetumia afisi yake kujinufaisha au kunufaisha mwingine kinyume cha sheria, anatenda kosa la matumizi mabaya ya afisi kama inavyoelezwa katika Kifungu cha 46 cha Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi,” alisema.

Iwapo mswada huo utakubaliwa na kuchapishwa, Bw Waluke amesema atapendekeza mabadiliko zaidi ya kuhakikisha wahasibu wa shule za umma wanahamishwa kila baada ya miaka mitatu

“Wahasibu ni kama watumishi wa umma; kwa nini wahudumu shule moja milele? Hapo ndipo rushwa huzaliwa na mali ya umma kutumiwa vibaya,” alisema.

“Watu hawa wameharibu shule nyingi. Wamepata mali kila mahali na hauwezi hata kuelewa walizipataje,” aliongeza mbunge huyo.Kwa mujibu wa Bw Waluke, kuhusisha wake, waume na watoto katika ukaguzi huo ni njia ya kuzuia hali ambapo wahusika hutumia majina ya jamaa zao kuwekeza mali walizopata kwa njia za ufisadi.

Hata hivyo, mbunge huyo atalazimika kusubiri hadi Kamati ya Elimu ikamilishe uchunguzi wa pendekezo hilo la sheria kabla ya kumweleza Spika ikiwa mswada unastahili kuchapishwa rasmi na kuwasilishwa bungeni kwa hatua zaidi.

Iwapo kamati itapendekeza kuchapishwa, basi mswada utaanza safari rasmi ya kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni, kabla ya kupelekwa kwa ushiriki wa umma, ambao utaongozwa na kamati hiyo ya elimu.