Habari za Kitaifa

Pigo kwa Gachagua mwaniaji wake maarufu akiyoyomea kwa Moses Kuria

Na GEORGE MUNENE September 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua anaendelea kuona vimulimuli katika siasa za Mbeere Kaskazini baada ya mwaniaji aliyemtoroka kujiunga na Chama cha Kazi (CCK) chake Moses Kuria.

Duncan Mbui ambaye alitoroka DCP wiki jana sasa atawania kiti hicho cha ubunge kupitia CCK.

Wiki jana, Bw Mbui alitoroka DCP baada ya kubainika kuwa Bw Gachagua na vinara wenza kwenye upinzani, sasa wanamuunga mkono Newton Karish wa DP.

Kiti hicho kilikuwa kikishikiliwa na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku ambaye alichaguliwa kupitia DP mnamo 2022 na akahudumu hadi alipoteuliwa waziri.

Hatua ya Bw Mbui ambaye pia ni Diwani wa Evuvore kujiunga na CCK inatarajiwa kufungua uwanja mkali wa ubabe Mlima Kenya kati yake na Bw Kuria.

Kiongozi huyo wa CCK aliongoza mkutano mkubwa kwenye soko la Ishiara Jumanne ambapo alimkabidhi Bw Mbui cheti cha uteuzi kuelekea uchaguzi huo wa Novemba 27.

Bw Kuria alitoa wito kwa wapigakura wakatae kuwachagua viongozi kwa msingi wa kiukoo na badala yake waangalie maono na rekodi yao ya maendeleo.

Mambo ni mabaya zaidi kwa Bw Gachagua baada ya mwandani wake Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji kusema atauasi msimamo wa upinzani na kumuunga mkono Bw Mbui kwenye CCK.

Mbunge huyo alisema ilikuwa hatua ya kusikitisha kwa DCP kumkataza Bw Mbui atumie tikiti yake ilhali alikuwa ametumia rasilimali zake akivumisha chama hicho.

“Ninaamini kwenye usawa na nitasimama na Bw Mbui upande wowote wa kisiasa atauegemea,” akasema Bw Mukunji.

Wadi ya Evuvore anakotoka Bw Mbui ndiyo ina wapiga kura wengi zaidi kwenye eneobunge hilo.

Ikizingatiwa kuwa CCK ipo muungano wa Kenya Kwanza, kuna hofu kuwa atagawanya kura na mwaniaji wa UDA Leonard Muthende ambaye alitambulishwa wiki jana na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki.

Bw Muthende aliwania ugavana wa Embu mnamo 2022 lakini akabwagwa japo pia anasemekana kuwa na umaarufu sana katika siasa za Mbeere Kaskazini na Embu.

Kando na wawaniaji wa DP, CCK na UDA, Jubilee yake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta nayo imemsimamisha Jacob Ireri Mbao, mwaniaji ambaye ni kiziwi.

Wachanganuzi wa kisiasa wanasema uchaguzi huo ni kipimo cha umaarufu wa Bw Gachagua eneo la Mlima Kenya.

Kwa Profesa Kindiki, kura hiyo inatumiwa kupima iwapo anaweza kuelekeza kura za Mlima Kenya Mashariki kwa Rais William Ruto mnamo 2022.

Pia anatumia uchaguzi huo mdogo kuthibitisha kuwa bado anastahili kuwa mgombeaji mwenza wa Rais Ruto 2027.