Habari za Kitaifa

Pigo kwa Kidero korti ikiruhusu akaunti zake za benki zichunguzwe

Na SAM KIPLAGAT September 23rd, 2024 1 min read

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Evans Kidero amepata pigo baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali kesi ambayo alitaka kuzuia Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) kuchunguza akaunti zake za benki.

Majaji wa Mahakama ya Rufaa Daniel Musinga, Asike Makhandia na Sankale ole Kantai Jumatatu walisema maswali ambayo Dkt Kidero alikuwa akiuliza katika rufaa hiyo yamejibiwa na Mahakama ya Juu katika hukumu iliyotolewa katika kesi tofauti mnamo Februari 2019.

Kuhusiana na suala hilo, EACC inasaka habari zaidi kuhusu Dkt Kidero alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya sukari ya Mumias kati ya 2003 na 2012 na pia wakati wa uongozi wake kama gavana wa Nairobi.

Dkt Kidero alisema kwamba mamlaka ya EACC ni kutekeleza masharti ya Sura ya Sita ya katiba na hayahusu kuchunguza makosa isipokuwa yale yaliyotajwa katika katiba.

Alidai kuwa EACC ilivuka mamlaka yake ya kikatiba kwa kutaka kufanya uchunguzi dhidi yake baada ya kupata vibali vya kuchunguza akaunti zake sita za benki mnamo Februari 2016.

“Kwa hivyo inaonekana kuwa Mahakama ya Juu ilijibu malalamishi yote ya mlalamishi katika rufaa yake. Malalamishi hayo hayana msingi. Kwa hivyo, rufaa hii imetupiliwa mbali,” walisema Majaji Musinga, Makhandia na Sankale.

EACC ilipata maagizo ya mahakama kuchunguza stakabadhi za kufungua akaunti na shughuli zote zinazohusiana na akaunti za benki za Dkt Kidero.