Habari za Kitaifa

Pigo kwa Kingi vigogo wa PAA wakirudi ODM

January 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na NDUBI MOTURI

SPIKA wa Seneti Amason Kingi Alhamisi, Januari 18, 2024 alipata pigo kuu kisiasa baada ya waanzilishi wa chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA) kuhamia chama cha ODM.

Kinara wa Upinzani Raila Odinga aliwapokea wanachama hao wa PAA na kuwakaribisha rasmi ndani ya chama chake.
Hafla hiyo ilifanyika katika makao makuu ya ODM, Chungwa House, Nairobi.

Waanzilishi waliogura PAA walijumuisha kiongozi wake wa vijana katika Kaunti ya Kilifi Samir Nyundo.

Bw Nyundo alikuwa kiongozi wa vijana wa ODM Kilifi kabla ya kuhamia PAA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Akiongea wakati wa hafla hiyo, Bw Nyundo alijutia kuhamia PAA, akaomba msamaha, na kumshutumu Spika kwa kuwachongea viongozi chipukizi ambao anawaona kama washindani wake wa kisiasa.

“Tulibuni chama hiki tukijua kuwa tulikuwa tunamuunga mkono Bw Odinga ila kiongozi wa chama chetu akajiunga na Kenya Kwanza. Hatukuwa na jingine wakati huo japo uamuzi wake huo ulitushangaza,” akasema Bw Nyundo.

“Alitumia chama kujinufaisha na baada ya kupata wadhifa wake, hajawahi kushughulika na hata kuulizia chama kinaendeleaje. Hiyo ndiyo maana baada ya kujisaili, tumeamua kurudi nyumbani,” akaongeza Bw Samir.

Wakati wa hafla hiyo, washirikishi wa masuala ya PAA Kilifi na Mombasa, waliwasilisha funguo kwa Bw Odinga, wakidai zilikuwa za afisi za chama cha PAA ambazo sasa wamezifunga na kurudi katika ODM.

Bw Odinga pia alishutumu Bw Kingi kwa kumhadaa kisiasa kisha kujiondoa ODM na kujiunga na Kenya Kwanza.

“Tulikuwa na mkutano ambao ulidumu kwa zaidi ya saa tano katika afisi za ODM wakati ambapo alitaka kubuni chama chake na tulikuwa na gavana wa zamani wa Mombasa Hassan Joho.

“Ingawa nilikataa, tulimruhusu abuni chama hicho kwa masharti kuwa kitakuwa sehemu ya muungano wa Azimio. Bw Joho naye alisisitiza kuwa atasalia ODM.”

Huku akitafakari safari yake ya kisiasa na Bw Kingi, kiongozi huyo wa ODM aliwahongera viongozi hao, akisema kuhama PAA kulikuwa adhabu bora zaidi kwa Spika.

“Alikuwa wakili mdogo ndugu yake alipomjulisha kwangu. Niliamua kumshika mkono na kumuunga mkono awe mbunge wa Magarini. Aliniambia alitaka kuwa Gavana wa Kilifi na nikampiga jeki kisiasa mnamo 2013 na 2017.

“PAA sasa imerudi nyumbani na sasa mwacheni yeye (Bw Kingi) abakie huko akiwa uchi.”

Wanasiasa wa Kilifi ambao waliwapokea viongozi hao pamoja na Bw Odinga ni Seneta Stewart Madzayo, Naibu Gavana wa Kilifi Flora Chibule, Mwenyekiti wa ODM Kilifi Teddy Mwambire, mbunge wa Magarini Harrison Kombe na mwenzake wa Malindi Amina Mnyazi.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna pia alikwepo. Bw Madzayo alisema eneo la Pwani ‘liko nyuma’ ya Bw Odinga kisiasa.

“Ninawashukuru mmeona nuru na kurudi nyumbani. Sasa muwe waaminifu kwa chama na mfuate tu mwelekeo ambao unatolewa na Baba (Raila),” akasema Bw Madzayo.