Habari za Kitaifa

Pigo kwa Korir mahakama ikakataa utetezi wake kuhusu ardhi tata

Na KEVIN CHERUIYOT July 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA imezima ombi la Katibu katika Wizara ya Ardhi Nixon Korir la kuzuia kuendelezwa kwa madai yanayomhusisha na ubadhirifu wa Sh2.7 bilioni, pesa zilizostahili kulipwa  wanachama wa kundi la makazi ya Dupoto ambao wanamiliki ardhi eneo la  Embakasi Kaunti ya Nairobi.

Kupitia uamuzi ambao ulitolewa mnamo Juni 30, Hakimu wa Mahakama ya Milimani Becky Cheloti alipuuza madai ya katibu huyo na kusema alikosa kuonyesha jinsi madai hayo yalivyomharibia sifa au kumchafulia jina.

“Ombi hili limeshindwa kudhibitisha maneno ya kuharibu sifa na haliwezi kuridhiwa. Kwa hivyo linatupiliwa mbali,” ikasema uamuzi huo.

Kwenye ombi hilo, Bw Korir alikuwa ameuliza mahakama itoe amri  Thomas Letangule, kampuni ya uwakili ya Letangule na Abdulhakim Dahir Sheikh, Dahir, Affey izuiwe kumhusisha na madai kuwa sehemu ya waliofuja pesa za kuwalipa wamiliki wa ardhi ya ekari 94 eneo la Embakasi.

Katibu huyo alidai kuwa mnamo Machi mwaka huu, alitumiwa barua mbili; Machi 7 na Machi 13 na kampuni hiyo ya uwakili.

Barua hizo pia zilinakiliwa kwa Tume ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC), Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Nchini (DCI). Barua hizo zilieleza kuwa alishiriki katika kutwaa kipande hicho cha ardhi kwa njia haramu.

Mapema mwaka huu, zaidi ya wanachama 300 wa kundi hilo la Dupoto kutoka jamii ya Maa waliandikia DCI kuhusu suala tata la umiliki wa ardhi hiyo.

Kundi hilo lilisema kuwa maafisa wa ngazi ya juu serikalini akiwemo katibu na Tume ya Kitaifa ya Ardhi Nchini (NLC) waliwahadaa ili waondoe kesi waliyowasilisha mahakamani mwaka jana.  Waliowahadaa walikuwa wameahidi kuwalipa zaidi ya Sh2.7 bilioni.

Licha ya pesa hizo kutolewa, wanachama hao 300 hawakupokea pesa zozote na wamekuwa wakizungusha tu. Wametishia kuwa watatwaa kipande hicho cha ardhi wasipolipwa hela zao.

Bw Korir alidai kuwa barua zilizoandikiwa afisi husika kuhusu suala hilo zilikuwa zikisambazwa mtandaoni na kummulika, akisema zimesababisha Wakenya wengi kutilia shaka maadili yake.

“Barua hizo zimeibua taswira hasi kuwa ni mtapeli, afisa wa umma fisadi na mkosa maadili ambaye anatumia afisi zake vibaya,” ikasema ombi la Bw Korir.

Hata hivyo Mabw Letangule na Abdulhakim walisema yaliyokuwa kwenye barua hiyo hayakumsawiri katibu huyo vibaya kivyovyote au kumharibia sifa.

“Barua hizo ziliandikiwa tu asasi za uchunguzi na hajatoa ushahidi unaonyesha kuwa alilengwa na sifa yake kuharibiwa,” ikasema stakabadhi za mahakama.