Pigo kwa madaktari wanaogoma Ruto akisema serikali haina pesa
NA CHARLES WASONGA
RAIS William Ruto amewaambia madaktari wanaogoma kwamba serikali haina pesa za kuwaongezea mishahara na marupurupu huku akiwataka warejee kazini.
Akiongea Jumapili, Aprili 7, 2024 baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa la African Inland (AIC) mjini Eldoret, Dkt Ruto alisema wakati huu serikali yake inakabiliwa na mzigo mkubwa wa gharama ya mishahara ya watumishi wa umma na haiwezi kujiongezea mzigo huo.
Hata hivyo, Rais aliahidi kuwa zaidi ya madaktari 1, 500 wanafunzi watapewa ajira.
“Tunawathamini zaidi enyi madaktari tunawathamini. Lakini hatuwezi kuwapa pesa ambazo hatuna kwani tunazongwa na gharama kubwa ya mishahara,” Dkt Ruto akaeleza.
Mgomo wa madaktari sasa unaelekea wiki yake ya nne huku chama chao (KMPDU) kikishikilia kwamba hakitasitisha mgomo hadi pale matakwa yao, kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano (CBA) yatakapoafikiwa.