Pigo kwa Ruto muundo wa ufadhili vyuoni ukizimwa
NI pigo kuu kwa Serikali ya Rais William Ruto baada ya Mahakama kuu kufutilia mbali mfumo mpya wa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu ikisema unabagua na kukandamiza haki wanafunzi kupata elimu muwafaka.
Akitangaza mfumo huu mpya uliozinduliwa na Serikali ya Kenya Kwanza unakiuka Katiba na haki ya watoto kupata elimu iliyo na ushindani katika lingo za kimataifa, Jaji Enock Chacha Mwita alisema matumaini na matarajio ya wanafunzi yalitiwa kiza.
Jaji Mwita alisema elimu ndicho kiungo muhimu zaidi katika ustawi wa kila nchi na kwanba ni jukumu ya Serikali kuhakikisha wanafunzi wamepokea elimu bora itakayowawezesha kubobea taaluma wanazohitimu.
Jaji Mwita alikubaliana na walalamishi walioishtaki serikali kwamba mfumo huu mpyawa kufadhili elimu katika vyuo vikuu umesababisha mtafuruku mkubwa katika fani ya elimu.
Jaji huyo alisema mfumo huu wa ufadhili wa elimu ya juu uliwatwika wazazi mzigo mzito wa kugharamia elimu ya wanao ambayo inapasa kugharamiwa na Serikali.
Mahakama ilikubaliana na Tume ya Kitafa ya Kutetea Haki za nadamu (KHRC), Elimu Bora Working Group na Miungano ya vyama vya wanafunzi kwamba mfumo huu unakinzana na Katiba kwamba serikali ifadhili masomo ya wanafunzi katika nyanja zote kwenye vyuo vikuu , taasisi za masomo ya anuai na kiufundi (TVETs).
“Mfumo huu mpya kufadhili elimu katika vyuo vikuu unakinzana na Katiba na unawabagua wanafunzi ambao wako na haki ya kupata elimu bora,”Jaji Mwita alisema.
Jaji huyo alisema Katiba imeipa serikali jukumu la kufadhili elimu katika vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi.
Alisema mwongozo wa serikali wa kuwajukumisha wazazi kugharamia elimu ya wanao ni “ukiukaji wa hali ya juu ya katiba na haki za watoto kupata elimu kwa ufadhili wa serikali.”
Jaji Mwita alisema wanafunzi kutoka familia sisizo na uwezo kifedha na wamehitimu kusoma taaluma zinazofadhiliwa kwa gharama ya juu wamebaguliwa.
Alisema lazima kuwe na usawa na haki itendeke kwa wote wanaofaulu kujiunga na vyuo vikuu.
Jaji Mwita alisema matarajio ya wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu kusoma taaluma waliohitimu yalikuwa yamedidimia.
Kabla ya mfumo huu kupitishwa na kuanza kutekelezwa , Jaji Mwita alisema haukupata uungwaji mkono na wananchi kwa kukumbatia maoni yao.
Jaji huyo alisema katiba imeshauri kwamba kabla ya mwongozo wowote ule au sheria yoyote ile lazima maoni ya wananchi yashirikishwe kabla ya kupitishwa na kuanza kutumika.
“Mchango wa umma kabla ya sheria au mwongozo kupitishwa lazima ushirikishwe,”Jaji Mwita alisema, huku akiongeza “maoni ya wananchi hayakushirikisha kabla ya kuanza kutumika.”
Baada ya maoni ya wananchi kusikika ilipasa bunge la kitaifa kuyajadili na kuyatathmini kabla ya sheria hiyo ya ufadhili wa masomo kufanyiwa mageuzo.
‘Ilipasa sheria hii na mfumo huu mpya wa ufadhili masomo uchangiwe na wananchi kabla ya kuanza kutekelezwa,” Jaji Mwita alisema.
Katika kesi hiyo iliyowasilishwa kortini mwaka uliopita, KHRC na mashirika hayo mengine yaliomba mahakama kuu iufutilie mbali mfumo huu hautilii maanani kamwe maslahi ya wanafunzi kutoka familia maskini.
Pia walalamishi walisema mfumo huu umezua mtafaruku katika uteuzi wa wananchi wanaojiunga na vyuo vya anuai na kiufundi (TVETs) kwa vile hakukuwa na mwelekeo kutoka taasisi ya uteuzi wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu (KUCCPS).
Pia KHRC ilisema “utaratibu wa utoaji mikopo ya ufadhili wa elimu ya juu haueleweki, umekumbwa na hali ya suinto fahamu na umekiuka sheria.’’
Jaji Mwita aliombwa afutilie mbali mfumo huu na kutupilia mbali tetezi za wizara ya elimu.
Mnamo Oktoba 3, 2024, Mahakama ilitoa agizo la muda kusitisha utekelezaji wa mfumo huu mpya wa ufadhili ya elimu vyuo vikuu.