Habari za Kitaifa

Polisi 200 wapelekwa Haiti kulinda usalama

May 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WANGARI

BAADA ya vuta nikuvute ya muda mrefu kortini, hatimaye kikosi cha kwanza cha maafisa 200 wa polisi kinatazamiwa kusafiri hadi nchini Haiti Alhamisi ijayo.

Kikosi hicho ni sehemu ya maafisa 1,000 walioidhinishwa na Umoja wa Mataifa kwenda kudumisha amani katika taifa hilo ambalo halijashuhudia utulivu kwa muda mrefu.

Kwa miezi kadhaa, serikali ilijipata ikipigwa mieleka na watetezi wa haki za binadamu, kuhusu azma yake ya kuwapeleka polisi katika nchi hiyo inayokumbwa na utovu wa usalama.

Machafuko nchini humo wakati mmoja yalimlazimu aliyekuwa rais, Ariel Henry kuzuru humu nchini na kutia saini mkataba maalumu.

Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, Rais Ruto alisema utawezesha kuharakisha oparesheni ya usalama ambayo imeibua matumaini Haiti ambapo machafuko yanazidi kuongezeka.

Hata hivyo, siku chache baadaye, mahakama iliubatilisha mkataba huo uliokuwa umesainiwa Oktoba mwaka jana baada ya kiongozi huyo kujiuzulu.

Licha ya pingamizi kali kutoka kwa wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu na mahakama nchini, serikali ya Kenya na Haiti zimeonekana kupania kusonga mbele na oparesheni hiyo inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na Amerika.

Taifa Leo imebaini kuwa, tayari Amerika imeanza kujenga kambi ambapo maafisa wa polisi Wakenya watakuwa wakiishi wakati wa oparesheni hiyo ya kuzima magenge ya waasi ambao wamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kusambaratisha amani nchini Haiti.

Kupitia oparesheni inayoongozwa na Kikosi cha Jeshi la Amerika, wanakandarasi kadhaa raia wametumwa kujenga kambi katika jiji kuu la Haiti, Port au Prince.

Kupitia taarifa iliyofikia Taifa Leo, Jeshi la Amerika lilisema wanakandarasi hao watashirikiana kwa karibu na maafisa wa uwanja mkuu wa ndege jijini humo kufanikisha oparesheni hiyo.

“Maafisa hawa watashirikiana na maafisa wa uwanja wa ndege Haiti kuimarisha ulinzi wa vifaa na bidhaa ambazo zimewasili Haiti,” Jeshi la Amerika lilisema.

Taarifa hiyo ilieleza vilevile kwamba, makundi mbalimbali ya raia wa Haiti wanaounga mkono oparesheni yamehakikisha usalama katika uwanja wa ndege licha ya mashambulio makali yanayoendelezwa na magenge yaliyojihami.

Japo oparesheni hiyo imeonekana kuibua matumaini miongoni mwa raia wa Haiti, hisia mseto zimeibuka kuhusu iwapo polisi Wakenya watafanikiwa kuzima magenge ya waasi na kurejesha amani na utulivu nchini humo.

Wadadisi wa masuala ya usalama wamekuwa wakijadili kwa kina kama polisi wetu wana uwezo wa kukabiliana na magenge, au hata kumaliza ghasia Haiti.

Waliotoa pingamizi walisema kizingiti kikubwa kitakuwa lugha. Idadi kubwa ya watu Haiti wanazungumza lugha za Creole na Kifaransa. Wengine huongea Kihispania na ni watu wachache mno wanaofahamu au wanaoweza kuongea Kiingereza.

Mbali na lugha, maafisa wetu wa polisi wamekuwa na sifa ya kupokea mlungula. Takwimu za Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kia mwaka zimekuwa zikiwaorodhesha polisi kuwa kati ya wafisadi nchini. Hili, huenda likalemaza misheni yake Haiti.

Polisi wa zamani Jimmy ‘Barbecue’ Cherizier, kiongozi wa genge la ‘G9’, ashika simu yake baada ya kuwahutubia wanahabari katika eneo la Delmas 6, Port-au-Prince, Haiti mnamo Machi 5, 2024. PICHA | REUTERS

Kinara wa magenge, Jimmy Cherizier, almaarufu ‘Barbecue’ Jumatatu aliambia redio NPR kwamba, wanasubiri kwa hamu kuwashinda polisi wa Kenya.

“Kama mwanamapinduzi wa Haiti Jean-Jacques Dessalines angekuwa muoga, watu wa Haiti hawangekuwa huru hii leo. Waleteni hao polisi. Tuko na hamu sana ya kumalizana nao,” akasema.

Ingawa Kenya ndiyo itakayoongoza ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa, mataifa mengine yanayotuma polisi ni Jamaica, Chile, Grenada, Paraguay, Burundi, Chad, Nigeria na Mauritius.