• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Polisi Kenya wanyaka raia wa Ethiopia wakiingizwa TZ kiharamu

Polisi Kenya wanyaka raia wa Ethiopia wakiingizwa TZ kiharamu

NA STANLEY NGOTHO

POLISI katika eneo la Loitoktok, Kaunti ndogo ya Kajiado Kusini, waliwazuia wahamiaji 90 wakiwemo watoto kutoka Nairobi waliokuwa wakivuka mpaka wa Tarakea Kenya-Tanzania.

Polisi waliambia Taifa Leo gari aina ya Isuzu nambari ya usajili KCB 548K lililokuwa likisafirisha raia wa Ethiopia lilinaswa na polisi kwenye kizuizi cha Imbirikani katika barabara ya Emali-Loitokitok mnamo Jumanne usiku.

Wakati wa msako, polisi walipata watu 90 wakiwemo watoto. Watu wazima wa kiume walikuwa 37 mkubwa akiwa na umri wa miaka 27 na watoto walikuwa 53 wa kati ya miaka 13 hadi 15.

Wahamiaji hao wanahusishwa na biashara ya ulanguzi wa binadamu.

Inaaminika walikuwa na mpango wa kuvuka hadi Tanzania kupitia mpaka wa Kenya kisha watafute njia nyingine za vichochoroni kuingia nchini Afrika Kusini.

Bado haijafahamika jinsi wahamiaji hao walivyoweza kufika Imbirikani kutumia barabara ya kutoka Nairobi yenye umbali wa kilomita 183 bila kutambuliwa.

Wageni hao wako kizuizini wakisubiri kuhojiwa zaidi huku dereva akifunguliwa mashtaka ya ulanguzi wa binadamu.

Gari hilo lilizuiliwa katika kituo cha polisi cha Imbirikani.

“Dereva alidai kuwa alipewa kandarasi na mtu asiyejulikana kutoka Nairobi kupeleka kundi la raia wa Ethiopia kwa mwanamume mmoja aliyetambulishwa kama Ken eneo la Loitoktok,” ilisoma ripoti ya daftari la Matukio katika kituo cha Polisi (OB NO) 05/19/ 02/2024.

Mpaka baina ya Kenya na Tanzania hivi karibuni umekuwa njia rahisi kwa biashara ya ulanguzi wa binadamu.

Mnamo Machi 13, 2023, raia wa Ethiopia walikamatwa baada ya kupatikana wakiwa wamejificha kwa pango eneo la Loitoktok.

  • Tags

You can share this post!

Teknolojia mpya ya PEM yatoa vipimo vya uhakika zaidi kwa...

Bondia anayeinukia Lamu afichua ‘bullying’ ilimzindua...

T L