Habari za Kitaifa

Polisi matatani kwa kudaiwa kuruhusu mauaji ya mshukiwa

March 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

MAAFISA watano kutoka kituo cha polisi cha Murang’a huenda wakakamatwa na kushtakiwa kuhusiana na mauaji ya mhudumu wa bodaboda Jumapili iliyopita.

Inadaiwa polisi hao walipanga njama na kuchangia mauaji ya mhudumu huyo Brian Muchiri kwa tuhuma za kuwa mwizi wa simu.

Mmoja wa polisi hao aliweka picha ya Muchiri akiwa ametiwa pingu mtandaoni na kuandika kuwa amemwonya mara kadha aache wizi.

Pia aliandika kuwa alale mahala pema kwenye jehanamu.

Kanda ya video ilionyesha polisi wakimsukuma Muchiri kwenye sehemu ya nyuma ya gari lao aina ya Landrover.

Baada ya hapo, walianza kushauriana na wanafunzi wa chuo waliokuwa wakimwandama mshukiwa badala ya kumtorosha.

Kisha walimfungua pingu na kumsukuma nje ya gari na kuwaacha wanafunzi hao wampige hadi akafa huku nao wakienda na gari lao bila kuchukua hatua zozote.

Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kainga Mathiu alisema suala hilo bado linachunguzwa na faili ya uchunguzi imefunguliwa.

“Uchunguzi unaendelea na matokeo yataonyesha jinsi mwanamume huyo alivyokufa na wale ambao walihusika na kifo chake watachukuliwa hatua kali,” akasema Bw Mathiu.

Mratibu wa masuala ya masilahi katika kamati wa wanabodaboda, Bw Stephen Mwangi, alidai kuwa afisa mmoja mwenye cheo cha juu aliwaagiza polisi hao wamwache Muchiri mikononi mwa umma ili auawe.