Habari za Kitaifa

Polisi sasa wagundua mbinu mpya zinazotumiwa na wauzaji chang’aa

April 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na STANLEY NGOTHO

POLISI wa Kitengela wamefichua mbinu fiche inayotumiwa na wauzaji pombe haramu ambapo wanatumia mikoba ya wanawake kupitisha chang’aa ili kukwepa mitego ya polisi huku kampeni ya kupambana na vileo hivyo ikiendelea.

Wakati wa msako wa polisi katika mtaa wa Noonkopir mnamo Jumanne jioni, polisi walipata lita 50 za chang’aa zikiwa zimefichwa ndani ya mkoba wa mwanamke katika nyumba moja ya kuuzia pombe.

Aidha, inasemakana kuwa wafanyabiashara walaghai huchuuza chang’aa iliyopakiwa katika karatasi za plastiki.

Polisi waliwataka wananchi kuwa waangalifu na kupekua mikoba mikubwa kupita kiasi inayobebwa na wanawake kwani huenda inatumika kusafirisha pombe haramu na mihadarati.

“Siku za nyuma wafanyabiashara walikuwa wakisafirisha chang’aa hadi Kitengela kwa kutumia magari. Tunafahamu kuwa wanawake sasa wanasafirisha pombe haramu kwa kutumia mikoba yao. Katika baadhi ya baa, mikoba ya wanawake hutumika kuwahadaa maafisa wa polisi,” akasema afisa msimamizi wa kituo cha polisi cha Kitengela David Ole Shani.

Aidha, afisa huyo alisema kwa maafisa wake wanawachunguza wahudumu wa bodaboda wanaoshukiwa kutumika kusafirisha chang’aa kutoka Nairobi hadi Kitengela.

Mnamo siku hiyo, maafisa wa polisi wakiongozwa na Ole Sani walinasa lita 100 za chang’aa zilizopakiwa katika karatasi za plastiki eneo la Migingo.

Aidha, watu kadhaa walikamatwa wakiwa walevichakari.

Mmiliki wa baa mbili katika ploti moja eneo hilo anayejulikana kama “Omosh” alifaulu kukwepa mtego wa polisi. Baadhi ya wabugiaji pombe waliopatikana katika eneo hili walikuwa wanawake ambwalioandamana na watoto wao wenye umri wa chini ya miaka 10.

“Katika eneo hili wanawake na vijana huendelea kujaa katika baa kubugia pombe licha ya msako unaoendelea. Idadi kubwa ya wanawake sasa ni waraibu wa pombe,” anasema Magdalene Mbatia ambaye ni mkazi.

Polisi walivamia kioski fulani cha kuonyesha filamu na kunasa misokoto 500 ya bangi.

Mmiliki wa kioski hiyo, mwanamume mwenye umri wa miaka 21, alimatwa kosa la kuuza dawa hiyo ya kulevya.

Wakazi wanataka msako uendelezwe ili kuokoa vijana wasiangamie katika lindi la utumiaji pombe na mihadarati.