Polisi wa trafiki hukusanya hongo ya Sh3 bilioni kila mwezi, yafichua EACC
AFISA Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Bw Abdi Ahmed Mohamud, ameelezea wasiwasi wake kuhusu kile ambacho kwa kawaida hujulikana kama ufisadi mdogo, akisema unaharibu nchi.
Mkuu huyo wa EACC anakadiria kuwa takriban Sh3 bilioni hukusanywa kama hongo kila mwezi na maafisa 1,000 wa polisi wa trafiki kutoka kwa madereva kote nchini.
Bw Mohamud alisema kuwa hongo ndogo zinazoitishwa na polisi wa trafiki, maafisa wa uhamiaji na maafisa wa serikali za kaunti kutoka watu wanaosaka huduma zinaumiza umma na zinakita mizizi ya ufisadi nchini. Alitahadharisha kuwa kuzipuuza ni kuruhusu madhara mabaya.
“Pesa tunazotoa kwa polisi wa trafiki waliokamatwa baada ya kufuatiliwa kwa saa mbili pekee ni takriban Sh20,000 ambazo wamekusanya kutoka kwa madereva. Hiyo ni takriban Sh3 milioni kwa mwezi kwa afisa wa polisi wa trafiki kila siku. Ukichukua idadi wastani ya polisi wa trafiki 1,000 unapata jumla ya Sh3 bilioni kwa mwezi,” alitanguliza Bw Mohamud.
“Lakini tunajua kuna zaidi ya maafisa 1,000 wa trafiki nchini. Hizi ni pesa nyingi zinazokusanywa kwa jina la hongo ndogo kutoka kwa Wakenya, lakini zina athari kubwa,” akaeleza.
Maafisa wa EACC wanasema ikiwa kila afisa wa trafiki aliyekamatwa alipatikana na Sh20,000 baada ya saa mbili pekee, ina maana kuwa wanaunda Sh100,000 katika saa 10 wakiwa kwa zamu yao kazini.
Kinara huyo wa EACC alisema uchunguzi wa tume umebaini hongo zinazochukuliwa na maafisa katika vituo vya kutoa huduma kama vile polisi, idara ya uhamiaji, serikali za kaunti zinaathiri mno jamii.
“Wakenya wanahisi athari za ufisadi katika maeneo ya utoaji huduma kwa sababu ni pesa zinazotoka moja kwa moja mifukoni mwao hata kama ni kiasi kidogo.
“Hii hutokea wanapotafuta huduma katika vituo vya polisi, Huduma Center, leseni za biashara, pasipoti, vitambulisho vya kitaifa na kadhalika. Kupuuza hongo hii ndogo kutasimika zaidi ufisadi ambao hatuwezi kuendelea kumudu kama nchi,” Bw Mohamud alieleza.
Afisa Mkuu huyo Mtendaji alisema hongo ya Sh100 inayotolewa kwa afisa wa trafiki na wahudumu wa matatu ili kupuuza makosa yoyote kwenye gari, huchangia kusababisha ajali na hivyo kupotea maelfu ya raia huku maelfu zaidi wakibaki na majeraha mabaya mno kuliko kiasi hicho cha ‘hongo kidogo’.
Haya yanajiri siku chache baada ya maafisa wa upelelezi wa EACC kuwakamata polisi wawili wa trafiki eneo la Kabete wakiwa na Sh40,000 kwenye operesheni kali kufuatia malalamishi ya umma.
Bw Mohamud alishangaza kufichua kwamba kwa jumla maelfu ya polisi wa trafiki hukusanya mamia ya mamilioni ya shilingi moja kwa moja kutoka kwa mifuko ya Wakenya.
Haya yanajiri siku chache baada ya maafisa wa upelelezi wa EACC kuwakamata maafisa wawili wa polisi wa trafiki eneo la Kabete na kupata Sh40,000 kutoka kwao wakati wa operesheni kali kufuatia malalamishi kutoka kwa umma.
Iliripotiwa kuwa washukiwa hao wawili kutoka kituo cha Polisi cha Kingeero walikuwa wakiweka kizuizi mara kwa mara katika eneo la Kibichiku, Kabete na kuomba hongo kutoka kwa madereva.
Katika kisa kingine, kufuatia malalamishi kutoka kwa waendeshaji magari na wanabodaboda kuhusu maafisa wa polisi wa trafiki kujipatia pesa kwa kisingizio cha kutekeleza sheria za trafiki katika mzunguko wa Globe Cinema, makachero wa EACC waliwakamata maafisa watatu wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Central wakiwa na Sh48,250 walizodaiwa kukusanya kwa saa mbili.
Maafisa watano wa polisi wa trafiki waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa kuitisha hongo.Bw Mohamud alitupilia mbali maoni ya Wakenya kwamba EACC inalenga zaidi kesi ndogo za hongo ikilinganishwa na kesi kubwa za ufisadi akisema zote zina athari mbaya katika utoaji wa huduma kwa raia.
“Kile Wakenya wanachukulia kuwa kesi ndogo za hongo za trafiki ni mbaya kama kesi kubwa za ufisadi na sisi kama Tume tunalenga kesi zote za ufisadi bila kujali asili yake kwa sababu athari yake ni mbaya. Hatutapuuza kesi yoyote ya ufisadi iwe ndogo au kubwa,” alisema.