Polisi wabobea katika ujambazi
INGAWA kwa maandishi mipaka ya kazi inayowekwa na Inspekta Jenerali wa Polisi kuhusu maeneo ya kaunti, tarafa au kanda inalenga kuweka mpangilio na uwajibikaji katika utekelezaji wa sheria, hali halisi ni tofauti.
Maafisa wa polisi wasio waaminifu wamechukulia mipaka hiyo kama mapendekezo tu ya kijuujuu, wakivuka maeneo ya wenzao kufanya uhalifu kama uporaji, utekaji na hata mauaji kwa manufaa yao binafsi.Afisa wa polisi anayehudumu kama Naibu OCS katika Kituo cha Polisi cha Kathonzweni, Kaunti ya Machakos, Bw Guyo Dida, tayari amekamatwa mara mbili kwa tuhuma za utovu wa nidhamu baada ya kuendesha shughuli za polisi katika Kaunti ya Nairobi bila idhini.
Mnamo Oktoba 2024, alikamatwa akiwa akiongoza trafiki katika mzunguko wa Bunyala, Nairobi bila kuidhinishwa. Alipatikana akiwa na kifaa cha mawasiliano kilichosajiliwa kutumiwa na Kitengo cha Polisi wa Kulinda Watalii.
Miezi mitatu baadaye, afisa huyo huyo alikamatwa tena kwa tuhuma za kuomba hongo na kumpiga mwenzake. Inasemekana alidai hongo ya Sh15,000 kutoka kwa dereva mmoja kwa tuhuma za kughushi kosa la trafiki ili kuachilia gari lake. Afisa mwenzake alipojaribu kuingilia kati, alishambuliwa pia.Dida alikabidhiwa kwa Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kathonzweni kwa hatua za kinidhamu.
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita pekee, maafisa 14 wa polisi na afisa mmoja wa magereza wamekamatwa kwa makosa mazito yaliyohatarisha maisha ya raia walioapa kuwalinda.Maafisa 10 kati yao wanatuhumiwa kufanya uhalifu mamia ya kilomita kutoka vituo vyao rasmi vya kazi.Maafisa sita waliokamatwa kutoka Migori ni washukiwa wa kesi ya wizi wa kimabavu, ambapo mfanyabiashara Elvis Musyoka alishambuliwa kabla ya gari lake aina ya Toyota Prado kuibwa.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, maafisa watatu kati ya hao ndio waliomshambulia Bw Musyoka, huku wengine watano wakihusishwa na kusaidia kuficha gari hilo kutoka kituo cha polisi cha Migori baada ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuanzisha uchunguzi.
Watatu wanaoshukiwa kumshambulia Musyoka pia wanahusishwa na mtandao wa unyang’anyi wa magari maeneo ya Kangundo Road, hasa Joska, viungani mwa Nairobi. Joska iko Kaunti ya Machakos, umbali wa zaidi ya kilomita 390 kutoka Kituo cha Polisi cha Migori.
Bw Musyoka amekuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa wiki mbili na anatarajiwa kushiriki katika zoezi la kuwatambua wahalifu mara atakapopata nafuu.Jumatano iliyopita, mahakama ya Nairobi iliagiza maafisa watano wa polisi na afisa mmoja wa magereza kuzuiliwa kwa siku 10 ili kuruhusu uchunguzi kuhusu biashara haramu ya silaha na risasi huko Turkana kukamilika.
Uchunguzi uliopelekea kukamatwa kwao unaonyesha afisa wa magereza Charles Ekidor Lotira alishirikiana na polisi wengine watatu — Isaac Kipngetich, Cyrus Kisamwa Ileli na Samson Muriithi Mutongu — kuwauzia majambazi silaha na risasi zilizonunuliwa kwa fedha za umma. Bw Lotira, Kipngetich na Ileli wanahudumu katika Kaunti ya Turkana.
Hata hivyo, Ileli ni msimamizi wa silaha katika ghala kuu la silaha la eneo la Industrial Area, Nairobi, umbali wa zaidi ya kilomita 630 kutoka Turkana. Bw Mutongu ni mtunza stoo pia katika Industrial Area.DCI ilisema kwamba, mafanikio yalipatikana baada ya Koplo Kipngetich kunaswa akiwa na risasi 1,000 kutoka kwa Ileli na Mutongu, mzigo ulionuiwa kumfikia ASP Ekidor Lotira.
Kesi hizi ni mfano tu wa tatizo sugu ndani ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ambalo limekuwepo kwa miaka mingi.Hata hivyo, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja anasema yeye na timu yake wanafanya kazi kuhakikisha mizizi ya uhalifu huo inang’olewa kabisa.
Kupitia msemaji wa polisi, Muchiri Nyaga, Bw Kanja alisisitiza kuwa maafisa wanaoendesha shughuli zao nje ya sheria ni wahalifu na watashughulikiwa kama wahalifu wengine.“Msimamo wangu ni kwamba, maafisa hao wasiotii sheria wako rumande kwa sasa.
Waliowakamata ni maafisa wenzao, jambo linalothibitisha wito wa kitaaluma wa maelfu ya wanachama wa NPS, na pia moyo wa kujitolea kwa ajili ya taifa,” alisema Bw Kanja kupitia msemaji huyo.Hata hivyo, Bw Kanja alikiri kuwa safari ya kusafisha huduma ya polisi maafisa wachache waovu itahitaji muda na juhudi endelevu.