Polisi wajivuta kuchunguza shambulio dhidi ya Gachagua: Siku nne sasa hakuna aliyekamatwa
SIKU nne baada ya shambulio dhidi ya aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua katika kanisa la ACK Witima, Othaya, Nyeri, ambalo ni tukio la hivi karibuni kati ya mfululizo wa visa 12 vilivyomlenga, hakuna mashahidi au washukiwa waliohojiwa au kukamatwa.
Viongozi wa usalama wamepuuza maswali mara kwa mara kuhusu hali ya uchunguzi wa ghasia zilizotokea mnamo Jumapili, ambapo wanaume waliokuwa na silaha na mavazi ya kawaida, wakisaidiwa na magari ya polisi, walinaswa kwenye picha na video wakifyatua risasi halisi na gesi ya kutoa machozi, huku wengine wakirusha mawe kuvuruga ibada.
Bw Gachagua na wafuasi wake walilazimika kutorokea usalama wao wakati wa kisa hicho ambacho viongozi wa kanisa, pamoja na Naibu wa Rais Kithure Kindiki na Waziri wa Ndani Kipchumba Murkomen, walikosoa, huku wakiahidi uchunguzi wa haraka na kufikisha wahalifu mahakamani.
Lakini siku nne baadaye, maafisa hawajatoa taarifa yoyote kuhusu jinsi uchunguzi unavyoendelea kama inavyofanyika katika visa vingine vinavyozua hasira ya umma.
Bw Murkomen jana alirudia kuwa kisa hicho kinachunguzwa.
“Nimewaagiza maafisa wa usalama wa eneo la Kati kuhakikisha kampeni za amani na kuacha mashambulio, hasa dhidi ya makanisa. Rais Ruto ametuagiza kuwa wavumilivu na mimi ninasema kama Waziri wa Usalama wa Ndani kuwa hii ni mara ya mwisho kushuhudia jambo kama hili,” alisema bila kutoa taarifa za hatua zilizochukuliwa.
Tangu Jumatatu, Taifa Leo imejaribu kuwasiliana na viongozi wa usalama kupata taarifa lakini hakuna majibu wanayotoa.
Miongoni mwao ni Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin, Mkurugenzi wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi Noordin Haji, na msemaji wa polisi Muchiri Nyagah.
Kulingana na taarifa zilizopatikana, shambulio la Jumapili liliandaliwa na baadhi ya maafisa wa polisi wakishirikiana na viongozi wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya.
Afisa mmoja alisema, “Tulikuwa polisi 15, tulipewa vijana 20 kuungana nasi Nyeri. Tulipewa maagizo kushambulia Bw Gachagua.”
Bw Gachagua amesema hajaitwa kuandikisha taarifa, na uchunguzi ulioahidiwa haujafanyika. Alikosoa Bw Murkomen kwa kutoa kauli za kisiasa zisizo na uwajibikaji.
Wengine, wakiwemo wanasiasa wa upinzani kutoka eneo la Mlima Kenya, wanasema visa hivi vinaonyesha ushirikiano wa wahalifu na baadhi ya maafisa wa polisi.
Viongozi wanasema ukimya huu wa taasisi za usalama unakiuka Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya Umma (2016), huku baadhi ya maafisa wa IPOA wakithibitisha maandalizi ya kutoa taarifa ya umma, lakini utekelezaji umechelewa.
Akizungumza katika Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe wa Chama cha DP jijini Nairobi jana, Bw Gachagua alimkosoa Bw Murkomen kwa “kutoa kauli za kisiasa zisizo na uwajibikaji”.
“Hatujajua ni nani aliyeagiza maafisa wa polisi waliokuwa na silaha rasmi na magari ya serikali kushirikiana na wahuni kutekeleza shambulio dhidi ya waumini,” alisema Bw Gachagua.
Hata hivyo, ilibainika kuwa Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) tayari ilikuwa imeandaa taarifa kwa umma lakini haikupata idhini ya kutoa taarifa hiyo.