Habari za Kitaifa

Polisi wakiri hawakutumia waliyojifunza Shakahola kuzuia mauaji Kwa Binzaro

Na  MISHI GONGO August 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IDARA ya Polisi nchini imekiri kwamba ilifeli kuchukua tahadhari kali zaidi kutokana na mauaji ya Shakahola, baada ya vifo vingine vilivyochochewa na itikadi kali za kidini kuibuka Kwa Binzaro katika Kaunti ya Kilifi.

Msemaji wa Polisi, Bw Michael Muchiri, alisema masaibu ya Shakahola ambapo zaidi ya miili 400 ilifukuliwa mwaka jana, yalipaswa kuwa funzo, lakini mapengo katika uratibu wa mashirika ya usalama yamesababisha historia kurudiwa.“Yalivyotokea Shakahola ni ya kuhuzunisha mno.

Tulidhani hali kama hiyo haitarudiwa. Lakini tumeshindwa kutumia mafunzo ipasavyo. Tungeboresha zaidi,” akasema Bw Muchiri wakati wa mafunzo ya uwajibikaji wa polisi mjini Mombasa.
Alisema kulikuwa na udhaifu mkubwa wa ushirikiano kati ya polisi, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), viongozi wa mitaa na jamii, hali iliyolegeza mwitikio wa usalama.

Bw Muchiri alithibitisha kuwa kitengo cha mauaji kimewekwa kuongoza uchunguzi wa Kwa Binzaro akikitaja kama dhehebu linaloendeshwa kwa siri na udanganyifu.“Bado hatujajua idadi kamili ya miili itakayopatikana. Hii ni hali ya kupotosha, kuosha akili na msimamo wa kimya unaozuia ukweli kujulikana,” akasema.

Kwa upande wake, Mamlaka ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) ilisema kushindwa huko hakukuwa jukumu la polisi pekee, bali ni la mashirika yote ya usalama.Mkurugenzi Mkuu wa IPOA, Elema Halake, alisema mashirika ya usalama hayakuchukua hatua za haraka kuzuia mauaji hayo mapya.

“Hitilafu hizi zinahusu polisi, kama msemaji alivyoeleza. Hii ni kushindwa kwa mashirika yote, kuanzia maafisa wa utawala hadi maafisa mashinani,” akasema Bw Halake.Alisema IPOA iliwaokoa baadhi ya waathiriwa kupitia ofisi yake ya Mombasa na kutoa mapendekezo kwa wachunguzi, lakini akasisitiza jukumu lao linamalizikia pale.

“Tulichunguza na kutoa mapendekezo. Ni wazi kulikuwa na kushindwa, na hilo halifai kusherehekewa,” akasema. Bw Halake aliongeza kuwa tayari IPOA imependekeza hatua zichukuliwe dhidi ya maafisa wakuu waliokuwa wakisimamia uchunguzi wa Shakahola na akasisitiza kuwa uwajibikaji kama huo utafuatwa pia kwa kesi ya Kwa Binzaro.

“Hili ni suala la kitaifa na tutaendelea kulifuatilia kwa karibu,” akasema. Hadi sasa, miili 32 na mabaki kadhaa ya kibinadamu yamepatikana katika msitu wa Kwa Binzaro, hali inayozidi kulinganishwa na mauaji ya kutisha ya Shakahola.