Polisi wamulikwa vikali kwa kukosa kukamata washukiwa waliomuua wakili Mbobu
MAAFISA wa upelelezi wanapigwa darubini vikali kwa kushindwa kumkamata mshukiwa hata mmoja kuhusiana na mauaji ya wakili Mathew Kyalo Mbobu, karibu siku 20 baada ya kuuawa kwa kupigwa risasi jijini Nairobi.
Mbobu aliuawa Septemba 9, na kadri siku zinavyosonga, hakuna mtu aliyekamatwa wala kufikishwa mahakamani kuhusiana na mauaji hayo.
Rais wa Chama cha Mawakili Kenya (LSK), Bi Faith Odhiambo, alisema hivi majuzi kwamba tofauti ya kasi ya uchunguzi kati ya mauaji ya Bw Mbobu na ya Mbunge wa Kasipul, Bw Ong’ondo Were, ni ya kusikitisha.
“Ndani ya wiki mbili tu baada ya mauaji ya Bw Were, waliowaua walikuwa tayari wamekamatwa na kufikishwa mahakamani. Tungetarajia hali kama hiyo kwa Bw Mbobu. Badala yake, familia yake imekuwa ikikumbana na hadithi za kusikitisha,” alisema Bi Odhiambo.
Taarifa ambazo Taifa Leo imepata zinaeleza kuwa maafisa wa Idara ya Mauaji ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamewatambua watu wasiopungua saba wanaochunguzwa kuhusiana na mauaji hayo. Wanaomulikwa ni pamoja na wanafamilia wake, wafanyakazi wake, na marafiki wa karibu aliowasiliana nao kabla ya kifo chake.
Mkurugenzi wa kampuni moja ambayo ilikuwa kwenye mzozo wa kisheria na marehemu pia anachunguzwa. Hata hivyo, vyanzo vya habari vimebainisha kuwa hadi sasa hakuna yeyote kati yao anayeaminika kuwa mshukiwa rasmi.
Uchunguzi unaonyesha kuwa wakili huyo alizungumza na watu wasiopungua 15 katika siku ya tukio, wakiwemo marafiki na wenzake kikazi. Maafisa wa upelelezi tayari wamepekua ofisi yake na kuchukua baadhi ya stakabadhi muhimu kwa uchunguzi.
Jumamosi, Taifa Leo lilimtafuta msemaji wa Huduma ya Polisi, Bw Michael Nyaga Muchiri, kuhusu maendeleo ya uchunguzi. Bw Muchiri alisema uchunguzi unaendelea na umepewa rasilmali na umakini wa kutosha.
“Jaribio lolote la kutoa hitimisho sasa litakuwa kikwazo kwa uchunguzi na halitasaidia,” alisema Bw Muchiri.
Mnamo jioni ya Septemba 9, 2025, Bw Mbobu aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye Magadi Road, Nairobi. Watu wawili waliokuwa wamepanda pikipiki walimvizia alipokuwa akiendesha gari pekee yake, na kumpiga risasi mara nane kwa karibu, tukio lililotajwa kama mauaji ya kikatili.
Mnamo Septemba 12, Kitengo cha Mauaji cha DCI kilichukua jukumu la uchunguzi. Watu watatu waliokuwa wamekamatwa awali kuhusiana na mauaji hayo waliachiliwa siku iliyofuata baada ya uchunguzi wa awali kuonyesha hakuna ushahidi wa kuwahusisha na tukio hilo.
Watu hao watatu walikuwa miongoni mwa waliokuwa wa mwisho kuonekana na marehemu kulingana na picha za CCTV. Hata hivyo, baada ya kuchunguza maelezo yao, timu ya DCI iliamua kuwa hakuna sababu ya kuwaweka kizuizini.
Mnamo Septemba 15, Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw Douglas Kanja, alisema kuwa maafisa walikuwa wamepata mwelekeo mpya katika uchunguzi huo. Alisema kuwa uchunguzi ulikuwa umefikia hatua ya juu, na baadhi ya watu walikuwa wakifuatiliwa kwa karibu.
Bw Kanja alielekeza Mkurugenzi wa DCI, Bw Mohamed Amin, kuharakisha uchunguzi na kuhakikisha haki inapatikana kwa haraka.
Hata hivyo, hakutaja muda maalum wa kukamilisha uchunguzi, akisisitiza kuwa kazi hiyo inahitaji umakini na muda wa kutosha.
“Tulianza kwa kuwakamata watu watatu lakini wakaachiliwa. Hivi sasa tunaelekea njia sahihi na tutawakamata wahusika halisi,” alisema Bw. Kanja.
Aliongeza kuwa ni vigumu kwa maafisa wa upelelezi kuendelea bila usaidizi wa raia, hasa mashahidi ambao hawako tayari kutoa taarifa muhimu.
Kwa upande wake, Bw.Amin alisema kuwa alikuwa ameunda timu maalum ya wataalamu wa upelelezi kutoka kitengo cha mauaji ili kuharakisha uchunguzi.
Alisema watu watatu waliokamatwa bado wanachukuliwa kuwa watu wa kufuatiliwa katika uchunguzi unaoendelea.
Bw. Amin alibainisha kuwa kuna hatua kubwa zilizopigwa katika kufichua waliomwua wakili huyo, lakini hakutoa maelezo zaidi akisema kuwa suala hilo ni nyeti.
“Mauaji ya wakili huyu tunayachukulia kwa uzito mkubwa. Tumetenga timu maalum kwa ajili ya kumsaka muuaji. Kuwakamata wahusika ni kipaumbele chetu,” alisema Bw Amin.