Habari za Kitaifa

Polisi wasaka mwanamume aliyetoa orodha ya anaolenga kuua

March 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

POLISI katika Kaunti ya Murang’a wanamsaka mfungwa za zamani ambaye ametoa orodha ya watu 10 anaopanga kuua katika kijiji anachotoka kilichoko kaunti ndogo ya Mathioya.

Kufikia sasa, mtu huyo anashukiwa kutekeleza mauaji ya watu wawili katika orodha aliyotoa.

Kulingana na mkuu wa polisi wa kaunti ndogo ya Mathioya Bw Antony Muriuki, mshukiwa alitoa orodha hiyo Ijumaa asubuhi katika kijiji cha Chui na anashukiwa alianza kutekeleza mpango wake mara moja kwa kuua wanaume wawili.

Orodha ambayo Taifa Leo iliona ina majina ya wanaume sita na wanawake wanne na kufuatia mauaji ya wawili wamebaki wanane, wawili kutoka kila jinsia.

Wale anaoshukiwa kuua walitambuliwa kama Stanley Kamau na Bernard Mahiu Mwangi, wote walio na umri wa miaka 44 na ambao hawakuwa wameoa.

Kinaya ni kuwa wawili hao waliuawa ndani ya kituo cha polisi cha Chui ambacho kilijengwa mwaka wa 2016 na hakuna afisa aliyewahi kutumwa kuhudumu hapo.

“Mshukiwa alijaribu kuua watu wengine wawili katika orodha hiyo- mwanamume na mwanamke- lakini juhudi zake ziligonga mwamba walipojifungia ndani ya nyumba zao, wakipiga nduru katika njia ambayo ilivutia wanakijiji na kumfanya atoroke,” alisema Bw Muriuki.

Bw Muriuki alisema kwamba mshukiwa anayesakwa anachukuliwa kuwa na “ wazimu, ni katili na hatari” na akawaomba watu katika kijiji hicho na maeneo jirani kuchukua tahadhari.

“Ni mtu aliyezoea kufungwa jela kwa jina Kariuki Wangumi mwenye umri wa miaka 52 ambaye alitoka jela mwaka wa 2022 baada ya kutumikia kifungo cha miaka saba kwa kuua mtu na mkewe katika kijiji hicho,” alisema.

Bw Muriuki alisema mshukiwa alitumikia kifungo chote na akaachiliwa huru kwa njia ambayo haikueleweka kwa kuua Keziah Muthoni na Joseph Geita—ambao walikuwa mtu na mkewe mwaka wa 2018.

Katika kisa cha Ijumaa, Bw Muriuki alisema mshukiwa alijaribu kuua kikatili watu wanne “ na tunaamini alifaulu kuua wawili na kushindwa kuwapata wengine wawili kwa kuvunja dirisha ya nyumba ya mwanamume mmoja aliyelenga ambaye alijifungia ndani.”

Mkuu huyo wa polisi alisema “ baada ya kushindwa kumpata mwanamume huyo kupitia dirisha, alikimbia hadi boma nyingine lakini mwanamke aliyelenga alikimbia na kujifungia ndani ya nyumba huku akipiga nduru”.