Polisi washtusha kwa ukatili wakizima fujo za maandamano ya Saba Saba
UKATILI wa polisi ulivuka mipaka wakikabiliana na waandamanaji Jumatatu ambapo zaidi ya watu 10 waliuawa.
Kote nchini, nyumba zimegeuka kuwa maeneo ya maombolezo, zikitikiswa na vilio vya watoto, wajane, na wazazi waliobaki kubeba machungu ya kuuawa kwa wapendwa wao.
Katika eneo la Kangemi, Nairobi, familia mbili zilipoteza wapendwa wao kwa njia ya kikatili mno. Elvis Musavi, mwenye umri wa miaka 25, na Paul Makori, mwenye umri wa miaka 37, walifariki kwenye barabara baada ya kupigwa risasi walipokuwa wakijaribu kusaidiana wakati polisi walipofyatua risasi kwa waandamanaji na waliokuwa karibu.
Musavi, aliyekuwa akielekea nyumbani kutoka kazi ya jua kali, alisikia kilio cha Makori baada ya kupigwa risasi mgongoni.
Alipoinama kumsaidia, risasi nyingine ilimpiga mgongoni wake sawa lile iliyomwangusha Makori.
Mtoto mwenye umri wa miaka 12, Bridget Njoki Wainaina, alipigwa na risasi ya polisi akiwa ndani ya nyumba yao huko Ndumberi, Kaunti ya Kiambu.
Njoki, ambaye hakuenda shule siku hiyo kutokana na taharuki iliyokuwa imesababishwa na maandamano ya Saba Saba ya Julai 7, alipoteza maisha baada ya kupigwa na risasi iliyofyatuliwa na polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari, mama yake alieleza jinsi tukio hilo la kusikitisha lilivyotokea.
“Ilikuwa saa kumi na mbili jioni tuliposikia mlipuko mkali. Nilipomwangalia binti yangu, niliona damu mikononi mwake. Mwanzoni nilidhani alikuwa amejikuna au kupigwa na kitu, lakini nilipotazama kwa makini niliona ana tundu kichwani. Hapo ndipo nilipopiga kelele kuomba msaada, na baba yake akaingia,” alisimulia mama huyo kwa uchungu.
Familia ya Brian Kimutai, mwandamanaji mwenye umri wa miaka 21, aliyedaiwa kupigwa risasi na afisa wa polisi wakati wa maadhimisho ya Saba Saba huko Kitengela, ilikwama na mwili wake ndani ya gari katika mochari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kitengela kwa saa 14 baada ya usimamizi wa hospitali hiyo kukataa kuupokea mwili huo.
Brian, ambaye alikuwa mwendesha bodaboda, alitangazwa kufa alipofikishwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kitengela, ambako alikimbizwa wakati wa maandamano ya Jumatatu yaliyotikisa mji huo.
Baadaye, waandamanaji waliokuwa na hasira walizingira hospitali hiyo kwa takriban saa tano wakijaribu kuwazuia maafisa wa polisi kuufikia mwili huo.
Jioni, familia ikisaidiwa na waandamanaji walichukua mwili kwa gari la binafsi hadi nyumbani kwao, umbali wa mita chache kutoka hospitali hiyo.
Jana asubuhi, familia ilirudisha mwili huo katika mochari ya hospitali hiyo lakini usimamizi wa hospitali ulikataa kuupokea mwili huo, hali iliyosababisha mvutano.
Mwili huo, uliokuwa umefungwa kwa mashuka, ulikuwa katika kiti cha abiria cha gari aina ya station wagon.
Bi Ann Nyawira Gikunju, mama ya Brian, aliambia gazeti la Taifa Leo kuwa aliamua kuuchukua mwili wa mwanawe nyumbani baada ya kupata habari kuwa maafisa wa DCI walikuwa na mpango wa kuuhamisha hadi mochari ya jiji bila ruhusa yake.
“Tulikesha na mwili ukiwa ndani ya gari usiku kucha kwenye egesho la nyumba ya kupanga. Hatukuweza kuwaruhusu polisi waupeleke mochari ya mbali,” alisema Bi Gikunju.
“Maafisa wa polisi wananisumbua baada ya kumuua mwanangu. Nitapigania haki yake hadi mwisho,” aliongeza.
Mama huyo alisema mwanawe alikuwa mhanga wa uhasama wa kibinafsi kati yake na afisa wa polisi aliyempiga risasi, akidai kwamba alikuwa ametishiwa na afisa huyo aliyefahamika.
“Tulihisi kuwa polisi walitaka kuchukua mwili ili kuharibu ushahidi. Hatukuweza kuwaruhusu. Ndiyo maana tuliamua kuuondoa mwili hospitalini usiku wa Jumatatu,” aliongeza.
Baada ya mvutano wa takriban saa mbili, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walipoukagua mwili huo, ulihamishiwa mochari ya Hospitali ya Shalom, Athi River, Kaunti ya Machakos.
Hayo yalijiri huku polisi wenye kiu ya damu wakiangamiza watu zaidi ya kumi Julai 7, waliouawa kwa kupigwa risasi katika maeneo mbalimbali ya nchi wakati wa maandamano ya kuadhimisha miaka 35 ya Siku ya Saba Saba.
Watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi eneo la Kangemi kwenye barabara ya Waiyaki Way jijini Nairobi, ambapo wengine watatu walijeruhiwa vibaya kwa risasi.
Kwa mujibu wa shahidi, mmoja wa waliopigwa risasi Kangemi hakuwa miongoni mwa waandamanaji, bali alikuwa mkazi aliyekuwa akielekea nyumbani kutoka kazini alipopigwa na risasi kiholela.
Ripoti zinaonyesha kuwa waandamanaji wengine watatu waliuawa kwa risasi huko Ngong, Kaunti ya Kajiado, polisi walipokuwa wakitawanya umati wa watu waliokuwa wamefunga barabara katika eneo hilo.
Mfanyabiashara mmoja mwanamke alipigwa risasi na kuuawa mjini Nakuru wakati polisi walipokuwa wakikabiliana na washukiwa wa uporaji.
Afisa wa matibabu katika zahanati ya Eagle Nursing Home huko Kangemi, Dkt Aron Sikuku, alisema kuwa walipokea miili miwili, yote ikiwa na majeraha ya risasi.
Huduma katika zahanati hiyo zilitatizika kwa muda baada ya mamia ya waandamanaji kuvamia kituo hicho wakitaka kuondoa miili hiyo.
Wengi wa waandamanaji waliojeruhiwa hawakuweza kupata huduma za dharura za matibabu kwa sababu barabara nyingi zilikuwa zimefungwa, jambo lililohujumu huduma za ambulensi.
Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) ilisema kuwa polisi wanaendelea kukaidi wazi agizo la Mahakama Kuu linalowataka maafisa wote wanaosimamia maandamano wawe katika sare rasmi na wawe wanatambulika wakati wote.
“Tume ilishuhudia maafisa wengi waliovaa kofia za kuficha sura, bila sare, wakisafiri kwa magari yasiyo na alama yoyote ya kuwatambua wakipiga doria katika kaunti za Nairobi, Kajiado na Nakuru,” KNCHR ilisema katika taarifa.
Aidha, tume ilisema kulikuwa na magenge ya wahalifu waliokuwa wakibeba silaha hatari kama mijeledi, marungu, mapanga, mikuki, na pinde na mishale katika maeneo ya Kisii Nairobi, Kiambu, Kajiado na Eldoret.
Hasa katika miji ya Nairobi na Eldoret, magenge yalionekana yakifanya kazi bega kwa bega na maafisa wa polisi.
Ripoti zilizotolewa na Kamati ya Usalama ya Kaunti ya Murang’a zilionyesha kulikuwa na hatari ya maandamano kukumbwa na ghasia.
Ingawa Kamishna wa Kaunti, Bw Joshua Nkanatha, alisisitiza kuwa mtu mmoja aliuawa na wengine 14 kujeruhiwa vibaya, ripoti ambazo bado hazijathibitishwa zinaweka idadi ya vifo kuwa watu saba.
Vyanzo huru kutoka Kamati ya Usalama ya Kaunti vilieleza kuwa watu sita walifariki katika maeneo ya Kigumo, Maragua na Kangema, huku Kandara ikiripoti kifo kimoja.
Hata hivyo, Bw Nkanatha alisema hawezi kuthibitisha idadi kamili ya vifo, akisema “tunaendelea kukusanya takwimu,lakini jambo moja ambalo lazima niseme ni kuwa polisi walifanya inavyostahili”
Wakazi walilalamika polisi walitumia nguvu kupita kiasi wakati wa kutuliza ghasia.
Bw Benjamin Kioko alisema polisi wa Murang’a ambao anawafahamu vyema walimuua kaka yake, Julius Muli Nduku, mwenye umri wa miaka 30 kwa kumpiga risasi katika soko la Kangari, alipokuwa akishiriki maandamano ya Saba Saba.
Paul Kagiri alikuwa akielekea nyumbani kutoka duka la video alipokuwa akitazama maandamano yaliyokuwa yakiendelea kote nchini alipokutana na mauti yake.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 ambaye hujipatia riziki kwa kufanya vibarua mjini Ngong, familia yake inasema hakuwa miongoni mwa waandamanaji.
“Hakuwa miongoni mwa waandamanaji. Lakini alipigwa risasi kutoka nyuma,” alisema baba yake mwenye huzuni, Stephen Mbugua.