Habari za Kitaifa

Profesa Mugenda asalimu amri, ajiuzulu bodi ya KUTRRH

Na STEVE OTIENO December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

PROFESA Olive Mugenda, Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH) amejiuzulu na kuondoka afisini mara moja.

Haya yanajiri siku moja baada ya wafanyikazi wa matibabu katika hospitali hiyo kususia kazi na kumtaka aondoke.

Akitangaza kujiuzulu kwake kutoka KUTRRH, Katibu wa Wizara ya Afya Harry Kimtai alisema kuwa Prof Mugenda aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu katika ofisi yake na kwamba aliwasilisha barua hiyo hiyo kwa Rais.

“Ofisi ya Rais imekubali kujiuzulu kwa Profesa Mugenda na kuagiza Bodi ya KUTRRH iundwe upya,” alisema.

Baadaye  notisi ya gazeti rasmi  la Kenya  ilitolewa kutangaza kuwa Rais William Ruto alikuwa amebatilisha uteuzi wa Profesa Mugenda na bodi ya hospitali hiyo.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali hiyo Isaac Kamau ambaye hivi majuzi aliteuliwa kushikilia wadhifa huo na bodi baada ya aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji Ahmed Dagane kutumwa kwa likizo ya kulazimishwa, aliagizwa kung’atuka na kuripoti  katika makao makuu ya Wizara ya Afya.

Dkt Dagane hata hivyo atasalia katika likizo yake ya lazima huku Katibu Kimtai akifafanua kuwa mkataba wake kama Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo bado haujakamilika na kwamba atasalia nje ya ofisi ili kupisha uchunguzi wa masuala yaliyosababisha kusimamishwa kwake na bodi iliyovunjwa.

Ili kuziba pengo lililobaki usukani wa taasisi hiyo, Katibu Kimtai alitangaza kwamba nafasi ya Bw Kamau itachukuliwa mara moja na Dkt Zainab Gura.

Katika hotuba yake ya kwanza, Dkt Gura alishukuru Wizara ya Afya kwa kumteua kuongoza KUTRRH na kuahidi kufanya kazi pamoja na wafanyikazi kuboresha hospitali hiyo.

“Nataka kuwahakikishia kuwa mimi ni msikilizaji na nitawasikiliza. Tafadhali mtupe usaidizi wa kutafakari na kutatua masuala tunaposubiri kupangwa upya kwa bodi. Ninatazamia kushirikiana nanyi. Natumai tutarudisha utukufu wa taasisi hii kuu,” alisema.

Kwa kuwa hakuna bodi ya kusimamia taasisi hiyo, katibu Kimtai alisema hospitali hiyo kwa sasa iko chini ya usimamizi wa Wizara na itashirikiana na Afisa Mkuu Mtendaji aliyeteuliwa  kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyikazi wa hospitali hiyo.

Mabadiliko haya yalijiri siku moja baada ya wafanyikazi wa KUTRRH kugoma  na kuandamana katika jengo la usimamizi wa hospitali hiyo. Waliibua masuala kadhaa, muhimu miongoni mwao yakiwa ni kutolipwa posho, bima ya matibabu na kutopandishwa vyeo.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA