PSC yakana kumuajiri Jacque Maribe katika wizara ya Kuria
NA WANDERI KAMAU
TUME ya Utumishi wa Umma (PSC) imepuuza ripoti kwamba imemwajiri mwanahabari Jacque Maribe kuwa mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Utumishi wa Umma.
Kwenye taarifa Alhamisi, mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Anthony Muchiri, alisema hakuna uteuzi kama huo ambao umefanywa na bodi haijapokea ombi lolote la kumwajiri Bi Maribe.
“Kwa kutoa ufafanuzi kamili, nafasi hiyo itajazwa kupitia utaratibu kamili wa uajiri ikiwa itatokea,” akasema Bw Muchiri.
Hilo linajiri wiki moja tu, baada ya ripoti kadhaa kudai kwamba Bi Maribe alikuwa ameshapata kazi hiyo.
Aliripotiwa kupata kazi hiyo siku chache tu baada ya kuondolewa shtaka la mauaji dhidi ya mfanyabiashara Monicah Kimani.
Alikuwa ameshtakiwa pamoja na mpenziye wa zamani, Joseph ‘Jowie’ Irungu, aliyehukumiwa kifo na Mahakama Kuu mnamo Jumatano kama adhabu ya kosa hilo lililotekelezwa mnamo Septemba 19, 2018.
Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, alikuwa amenukuliwa kwenye majukwaa kadhaa akithibitisha uteuzi huo wa Bi Maribe.
“Ni kweli kwamba (Maribe) amepata nafasi hiyo, ila aliteuliwa na PSC,” akasema Bw Kuria.
Baadhi ya washirika wa karibu wa Bi Maribe kama bloga Dennis Itumbi waliandika jumbe za kumpongeza kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa uteuzi wowote kufanyika serikalini, lazima PSC itangaze nafasi hiyo na baadaye kuwaorodhesha watu waliofikisha viwango vinavyohitajika kwa mahojiano.
Haieleweki ni kwa msingi gani Bi Maribe amekuwa akitia saini taarifa za mawasiliano kuhusu masuala tofauti kutoka wizara ya Bw Kuria.