Habari za Kitaifa

Quickmart yaomba msamaha, yachunguza madai ya mteja kudhulumiwa

Na CECIL ODONGO August 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

DUKA la jumla la Quickmart Jumanne lilimsimamisha kazi mmoja wa meneja wake na kuomba msamaha kuhusu tukio la mteja aliyekuwa amenunua maziwa kudhulumiwa.

Kupitia taarifa, usimamizi wa supamaketi hiyo ulisema kuwa umemsimamisha kazi meneja wa tawi lake la Buruburu ambaye anatuhumiwa kwa kumpiga  mteja, kisa kilichozua ghadhabu za Wakenya. Video iliyosambaa mitandano ilionyesha baadhi ya wateja wakidai kuwa wamewahi kuhangaishwa na meneja huyo.

Kutokana na kusambaa kwa video hiyo, kumekuwa na wito kuwa Wakenya wasusie supamaketi hiyo huku wengine wakitaka waheshimiwe na kusaka uwajibikaji kutoka kwa Quickmart.

“Tunawapa kipaumbele wateja wetu na heshima kwa kila mteja anayeingia mlango wetu. Tunasikitisha kilichofanyika na kumwomba msamaha mteja aliyeathirika pamoja na yeyote ambaye alikerwa na tukio lenyewe,” ikasema taarifa ya Quickmart.

“Punde tu baada ya kufahamishwa kuhusu tukio hilo, tulichukua hatua  kwa kumsimamisha mfanyakazi wetu aliyehusika huku tukiendeleza uchunguzi na asasi husika,” ikaongeza taarifa hiyo.

Quickmart ilitoa ufafanuzi zaidi kuwa imemfikia mteja aliyedhulumiwa na kumwomba msamaha kisha kuahidi kushirikiana naye wakati wa uchunguzi. Vilevile ilisema inamakinikia kuwa na mazingira maridhawa ya utendakazi kwa wafanyakazi na wateja wake.

Kwenye video iliyosambaa mitandaoni, mteja huyo alisimulia kuwa pamoja na ndugu yake, walijijazia maziwa baada ya kukosa mhudumu na wakalipa kisha kupewa risiti.

Walipokuwa wakiondoka walikabiliwa kwa nini walijijazia maziwa hayo  ambapo vuta ni kuvute ilifuata kisha meneja huyo akachukua risiti yao na kuirarua.

Meneja huyo aliwashangaza zaidi kwa kudai wawili hao walikuwa wameiba lita 57 za maziwa kisha kuwazuiliwa kwenye hifadhi ya supamaketi na kuwapiga.

“Tuliingiwa na wasiwasi na meneja huyo alituzuilia kisha akaanza kutupiga pamoja na ndugu yangu. Tulipomuuliza kwa nini alikuwa akitupiga, alikataa kujibu,” akasema mteja huyo.

Wawili hao kisha walipelekwa Kituo cha polisi cha Buruburu lakini baba yao alikuwa tayari huko na wakawaachiliwa.