Raia wa Somalia wafurika Mandera vita vikichacha Gedow
IDADI ya raia wa Somalia ambao wanasaka hifadhi Mandera inaendelea kuongeza huku vita kati ya wanajeshi wa Somalia na wanajeshi wa Jubbaland vikiendelea kuchacha eneo la Gedow.
Vita hivyo vilianza mnamo Julai 21 na vimechangia zaidi ya watu 2289 kutoroka Kenya kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Msalaba Mwekundu Mandera.
“Kuna maeneo mawili ambayo sasa yanatumiwa kuwapokea waliotoroka Somalia na sasa yanawasitiri zaidi ya watu 2,000. Wote ni wahanga wa vita Gedow,” akasema Adan Mustafa, Mshirikishi wa shirika la Red Cross Kaunti ya Mandera.
Shule za msingi za Barwaqo na Duse zinazopatikana Mandera zimegeuzwa vituo vya uokoaji.
“Wengi ambao wameathiriwa ni wanawake, watoto na watu ambao wanaishi na ulemavu. Makundi haya yote yanahitaji msaada wa kibinadamu,” akasema Bw Mustafa.
“Wanahitaji maji, huduma za kimatibabu, chakula na watoto wako katika hatari ya kupatikana na utapiamlo,” akaongeza.
Wakimbizi hao pia wanahitaji neti za kuzuia mbu, blanketi na makao.
“Kuna taharuki sana mpakani hata tunapoendelea kuwapokea wakimbizi mpakani. Tunatoa wito wa usalama kwenye mpaka wetu na maeneo ambako wakimbizi wanaendelea kusitiriwa,” akasema Bw Mustafa.
Shirika la Msalaba Mwekundu limekuwa likiwapa wakimbizi hao pia huduma za ushauri na nasaha.
Alipofikiwa, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Mandera Robinson Ndiwa aliwahakikishia wenyeji na wakimbizi kuwa usalama umeimarishwa Mandera.
“Tumeweka mikakati yote ya kiusalama kuhakikisha watu wetu wote ni salama na wale ambao watatoroka vita Somalia wanapata makao na huduma zifaazo,” akasema Bw Ndiwa.
Hata hivyo, kamanda huyo alisema mpaka wa kawaida kati ya Kenya na Somalia unaendelea kufungwa ili Alshabaab wasiingie nchini.
Somalia na Jubbaland zimekuwa na mzozo wa muda mrefu na kumekuwa na changamoto za kuhakikisha kuna usalama eneo la Gedow.
Mogadishu imekuwa ikishutumu Jubbaland kwa kuamrisha wanajeshi wake wavamie makao yake ya kijeshi na raia kwenye eneo la Bula Hawa. Uvamizi huo umechangia raia wengi kupoteza maisha yao.
“Watu wengi wamekufa tangu wiki jana. Biashara na nyumba zote zimeharibiwa na wapiganaji,” akasema Hawa Aden ambaye ni kati ya waathiriwa.
“Kuwa mkimbizi hakujawahi kuwa kwenye fikira zangu ila sasa nipo hapa naomba kuwe na utulivu ili nirejee nyumbani na kuendelea na kazi zangu kama hapo awali,” akaongeza.
Hawa Ali naye ameapa kuwa ataendelea kusalia Kenya hadi usalama uiimarike nyumbani.
“Nashukuru kwa msaada na jinsi ambavyo nimepokelewa hapa Kenya. Nitaishi hapa hadi hali irudi kawaida nyumbani,” akasema.
Mnamo Jumatano kulikuwa na vita vikali Bula Hawa ambapo makombora yaliyorushwa yalianguka hadi Mandera.