Raia walia hali ya demokrasia nchini -Ripoti
ZAIDI ya nusu ya Wakenya hawaridhishwi na hali ya demokrasia nchini kutokana na visa vya utekaji nyara wa wakosoaji wa serikali, kutoheshimu uhuru wa kujieleza na uongozi mbaya.
Utafiti mpya wa Muungano wa Mashirika ya Kijamii ya Kutetea Ugatuzi, umeonyesha kuwa asilimia 65 ya Wakenya hawaridhishwi na kuzorota kwa mazingira ya kidemokrasia nchini, wengi wao wakihofia kukosoa serikali wakiogopa kulengwa na kuteswa.
Ni asilimia 21 pekee ya Wakenya walioonyesha kuridhika na hali ya sasa, huku asilimia 13 wakisema hawana msimamo kuhusu suala hilo.
“Sababu kuu zilizotolewa na wananchi kuhusu kutoridhishwa kwao na demokrasia ni uongozi duni, utekaji nyara wa wakosoaji wa serikali na uhuru wa kujieleza kutoheshimiwa,” inasema ripoti kuhusu utafiti huo uliofanyika kati ya Machi 3 na Machi 30, 2025.
Wananchi walioshiriki walisema wanaamini ni haki yao kukosoa serikali na kwamba demokrasia na haki ni muhimu hata kama maendeleo hayapatikani.
Katika kipindi hiki cha kuelekea kwa kongamano la ugatuzi, matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa asilimia 74.2 ya Wakenya wanapinga uamuzi wa serikali ya kitaifa kuzima fedha kwa majukumu yaliyogatuliwa.
Aidha, asilimia kubwa zaidi ikiwa ni 76.7 wanataka fedha hizo ziachiliwe mara moja ili kaunti ziweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mahitaji ya wenyeji.
“Kongamano lijalo la ugatuzi ni nafasi nzuri ya kutathmini hali ya demokrasia yetu, utiifu kwa utawala wa sheria na zaidi ya yote, hatua tulizopiga kama taifa katika safari ya ugatuzi. Kama mashirika ya kijamii, tutatoa kwa uwazi changamoto zinazokumba ugatuzi na njia za kuzitatua,” alisema Bw Evans Kibet, Mratibu Mkuu wa Kenya Devolution Sector Working Group.
Ripoti hiyo pia inaonyesha imani duni ya Wakenya katika vita dhidi ya ufisadi, ambapo asilimia 68.7 wamesema hawaridhishwi na usimamizi wa rasilimali za umma nchini.Asilimia 76 walisema hawana imani kuhusu uwazi katika utoaji wa kandarasi, na asilimia 74.3 kuhusu juhudi za kupambana na ufisadi.
Asilimia 72.4 ya Wakenya walisema wameshuhudia visa vya hongo au matumizi mabaya ya rasilimali serikalini, na asilimia 76.1 katika kiwango cha kaunti, asilimia 63 ya walioshuhudia hawajawahi kuripoti visa hivyo.
Hatua hiyo ya watu kutoripoti visa hivyo, inahusishwa na hali ya watu kutoamini mifumo iliyopo na hofu ya kulipiziwa kisasi.Matokeo ya utafiti pia yanaonyesha kuwa asilimia 30 ya Wakenya wana imani kuu kuwa kizazi cha Gen Z kitawatetea Wakenya kuliko taasisi za jadi kama vile mahakama, polisi, bunge, rais na vyama vya kisiasa.
Asilimia 14 walisema kuwa Gen Z ndio kundi linaloaminika zaidi kwa ujumla. Data ya utafiti huo ilikusanywa kati ya Julai na Agosti 2025 kwa washiriki 1,990.