Habari za Kitaifa

Raila aahidi kutekeleza ndoto za Gaddafi huku akiimarisha kampeni za AUC

Na JUSTUS OCHIENG November 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAONO ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ya kuunganisha nchi za Afrika yanaendana na aliyekuwa ya Rais wa Libya, Muammar Gaddafi.

Marehemu Gaddafi aliwahi kupigia debe wazo la kubuniwa kwa ‘Muungano wa Mataifa ya Afrika’ (United States of Africa) ili kuimarisha uchumi na umoja wa bara.

Mnamo Ijumaa, akiwa Addis Ababa, Ethiopia, Bw Odinga alitilia mkazo hitaji la umoja anapowania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

“Nina maono makubwa kwa Afrika; bara lenye umoja, mshikamano, utajiri na amani,” akasema Bw Odinga.

“Umoja wa Afrika ni muhimu sana kwangu. Lazima turejeshe umoja ili uwe kipaumbele kama walivyofanya Mwalimu Nyerere na Nkrumah,” akaongeza.

Lengo la Bw Odinga ni kama la Bw Gaddafi alipoanza kushinikiza nchi za Afrika kuungana kuanzia 1997.

Mnamo Julai 1999, Bw Gaddafi alisukuma mshikamano zaidi kwa mataifa ya Afrika katika masuala ya siasa na kiuchumi alipohutubia Kongamano la Shirika la Umoja wa Afrika (OAU) ambalo sasa linaitwa Tume ya Muungano wa Africa (AUC).

“Lazima tubuni bunge la kiafrika na benki. Bunge hili litapiga jeki azma ya bara kuungana huku benki ikiharakisha utekelezaji wa mikataba ya kuunda jumuiya ya kiuchumi Afrika,” alisema Bw Gaddafi.

Kati ya mwaka wa 1999 na 2002, Bw Gaddafi alikuwa mstari wa mbele katika kuimarisha OAU hadi ikapata katiba mpya na kubadili jina kuwa Muungano wa Afrika (AU).

Je, msukumo mpya wa Bw Odinga kuunganisha Afrika utazaa matunda? Na Je, kiongozi huyu mashuhuri atafaulu pale ambapo Bw Gaddafi alifeli?

Katika mahojiano na mwenyekiti mwenza wa kikosi cha kampeni ya Bw Odinga, Balozi Elkanah Odembo mnamo Jumapili, alifichua kuwa maono ya Bw Odinga yanaakisi yale ya Bw Gaddafi.

“Bw Odinga anaamini iwapo Afrika haitazungumza kwa sauti moja, bara halitakuwa na nafasi katika ngazi ya kimataifa,” akasem Bw Odembo. “Sababu ya utajiri wa Afrika, lazima tuelewe kuwa nguvu yetu iko katika umoja wetu,”

Akikutana na washirika wa AU Addis Ababa mnamo Jumamosi, Bw Odinga alivumisha haja ya utekelezaji wa Ajenda ya Afrika ya 2063.

Ili kuongeza matumaini ya Bw Odinga, kikosi chake kimepanga kampeni ya ‘nchi hadi nchi wakilenga kukutana na marais wa Afrika kuanzia juma lijalo ili wampigie kura Februari 2025.

“Mlimsikia akisema karibu asilimia 95 ya maazimio hayajatekelezwa. Raila Odinga anataka kuondoa vizuizi hivyo vyote kwa kushirikiana na kila kiongozi,” Bw Odemba aliambia Taifa Leo.

Bw Odinga ana azma ya kuimarisha uchumi, miundomsingi na kuoanisha sera mbalimbali badala ya muungano wa moja kwa moja wa kisiasa.