Raila ahofia Kenya kuwa ‘Taifa la Majambazi’ utekaji ukiendelea
ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga anamtaka Rais William Ruto akomeshe utekaji nyara wa Wakenya akisema nchi haifai kuwa ‘taifa la majambazi.’
Katika mahojiano ya kipekee katika Runinga ya Citizen Ijumaa usiku, Kiongozi wa Upinzani alisema utekaji nyara unaenda kinyume cha Katiba.
“Ni kama nchi ya majambazi ambapo unawaona watu wachanga wakitekwa nyara na watu wenye ujasiri. Wanakaa kama maafisa wa polisi wanaovaa mavazi ya kiraia lakini wanajua wanachokifanya wakiwateka nyara watu na kuwatesa,” akasema Bw Odinga.
“Wana pingu – hizi si bidhaa ambazo unaweza kununua kutoka madukani. Pingu ni maalum na humilikiwa na serikali,” akaongeza akifananisha matukio haya na hali inayoendelea Haiti ambapo majambazi wanavuruga nchi hiyo.
Bw Odinga alihofia nchi inaweza kurudi nyuma katika enzi za utekaji nyara na mateso wakati marehemu Rais Daniel Moi alikuwa kiongozi wa nchi.
“Walikuwa wanakamata watu, kuwafunga macho, kuwatupa ovyovyo ndani ya gari na kuwapeleka hadi Nyayo House (katika chumba cha kuwatesea watu). Wanakuweka katika seli yenye maji baridi sana… Tulidhani enzi hizo zimefika mwisho,” akasema Bw Odinga akieleza mateso aliyopitia miaka ya 80 alipokosoa serikali.
“Nilipitia haya na sitaki visa hivi virejee tena. Sitaki kuona watu wakiteswa kwa sababu ya kuwa na misimamo tofauti,” akaongeza.
Bw Odinga alishauri serikali ikabili visa tata kuhusu utumiaji wa mitandao ya kijamii kwa njia ya kisheria.
“Hii ni hali halisi ya maendeleo ya kiteknolojia na tunafaa kuikumbatia na kutafuta jinsi ya kuishi katika jamii yenye uwiano,” akaeleza Bw Odinga.
Mnamo Ijumaa, Rais Ruto aliahidi serikali itamaliza visa vya utekaji nyara akiwataka wazazi kuchukua jukumu la kuwalea watoto wao wawe raia wema.
Alisema haya alipohudhuria fainali ya mashindano ya Genowa Governor’s Cup 2024 katika Uga wa Raila Odinga Kaunti ya Homa Bay akiandamana na Bw Odinga na Gavana Gladys Wanga.
Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja alipinga madai kuwa maafisa wa polisi wanahusika katika utekaji nyara wa wananchi kupitia taarifa ya Desemba 26, 2024.